Na Bigambo Jeje, Musoma.
Kiwanda
cha kusindika maziwa na maji cha Mara Dairy kilichopo mjini Musoma mkoani
Mara kimeanza kujipanga kukabiliana na
ushindani wa soko la maji ya kunywa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa kuendelea kuzalisha bidhaa bora sanjari na kutumia bidhaa za kiwanda hicho
kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo
hapa nchini.
Moja ya mkakati ulioanzishwa na kiwanda
hicho katika kukabiliana na ushindani wa soko la bidhaa hiyo katika nchi za EAC
ni kubadili jina la maji toka Super Water na kuwa Serengeti ambayo ni moja ya
hifadhi kubwa ya wanyama katika bara la Afrika na iko kwenye maajabu saba
duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho cha
Mara Dairy James Mathayo anasema wamefikia uamuzi huo kubadili jina toka SupperWater
hadi Serengeti kwa sababu kadhaa ikiwemo hiyo ya kuukabili ushindani baada ya
soko la bidhaa hiyo kuanza kudorola ndani ya kipindi cha takribani miaka 5
iliyopita.
“ Tulipoanza kusindika maji yalikuwa na
rangi ya kijani hivyo kutokana na hali ya kisiasa hapa kwetu mkoani Mara
walianza kuyaita maji ya Chama cha CCM na hatua hiyo kusababisha soko kushuka
kwa kiasi kikubwa na ndipo mwaka wa jana wa 2015 tukaamua kubadili jina na
kuyaita Serengeti,” Anasema.
Mathayo anasema uamuzi huo sasa una
faida kubwa katika kukuza utalii na uchumi wa nchi kwa vile maji hayo
yanatangaza hifadhi ya wanyama ya Serengeti kwa watalii na wageni toka nchi
mbalimbali duniani wanaoitembelea hifadhi hiyo kwa shughuli za utalii
unaoliingizia serikali pato la watani dola bilioni mbili kwa mwaka sawa na
zaidi ya sh bilioni 4 .
Anasema maji hayo ya Serengeti sasa yana
mwitikio mkubwa wa soko ambapo idadi kubwa ya watalii wanaotembelea hifadhi
hiyo wameonekana kuyapenda sana kutokana na kuwa na jina sawa na hifadhi ya
Serengeti sanjari na bia ya Serengeti inayouzwa kwa wingi hifadhini humo.
Anasema mbali na uzalishaji wa maji ya
Serengeti, kiwanda chake pia kwa muda wa miaka mingi kimekuwa kikizalisha na
kusindika maziwa ya Mara ambayo yamejizolea soko katia nchi za Tanzania na Kenya
kutokana na ubora wake hususani maziwa ya mgando aina ya Yogurt yanayotokana na
ng’ombe wa asili toka wilaya za Musoma,Butiama,Bunda,Tarime,Rorya na Serengeti.
Mkurugenzi huyo Mtendaji huyo wa kiwanda
hicho anatabaisha kwamba kutokana na uzalishaji unaofanywa na viwanda vingi vya
bidhaa za hapa nchini na kuuzwa katika soko lenye ushindani la Jumuiya ya
Afrika Mashariki kunaondoa dhana potofu iliyojengeka kwa baadhi ya
wafanyabishara toka nchi wanachama kuwa Tanzania haina cha kuuza katika soko
hilo.
“ Si kweli kwamba Tanzania haina cha
kuuza na kwamba imekuwa dampo kwa bidhaa za nchi wanachama, kwa mfano katika
kipindi cha mwaka 2010 mauzo ya bidhaa zetu za hapa nchini yaliongezeka hadi
kufikia dola za Kimarekani milioni 462.7 kutoka dola za Kimarekani milioni
285.0 mwaka 2009, sasa anawezaje kusema kuwa nchi yetu ni dampo?” anasema na
kuongeza kuwa,
“ Ongezeko hilo lilikuwa ni sawa na
asilimia 62.3. na kwa miaka ya karibuni
mauzo hayo yamezidi kuongezeka kwa kasi. Kenya imeendelea kuwa soko kubwa kwa
bidhaa za Tanzania ikiwa inachukua asilimia 60.6 ya mauzo yote ya bidhaa za
hapa nchini ndani ya Jumuiya hiyo hukubaadhi ya bidhaa zilizouzwa kwa wingi
kutoka Tanzania kwenda Kenya kwa kipindi hicho kuwa ni pamoja na vyandarua,
bidhaa za plastiki, chai, transfoma, karatasi na bidhaa za karatasi”.
Mathayo anasema si kweli kuwa Tanzania ni dampo
katika soko hilo kwa vile anakumbuka katika kipindi hicho cha miaka mitano
iliyopita bidhaa nyingine zilizouzwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
ni mbolea, saruji, mchele, chuma, samaki, ngano, sukari na nguo.Vile vile Urari
wa biashara uliimarika kutoka nakisi ya Dola za Kimarekani milioni 31.9 mwaka
2009 hadi kufikia urari chanya wa Dola za Kimarekani milioni 168.8 katika mwaka
2010.
Anafafanua kuwa takwimu za mwaka 2011 zinaonesha
Tanzania ilikuwa na urari chanya wa dola za Kimarekani milioni 30.9 hivyo tokea
mwaka 2009 ambapo biashara ya Tanzania ilishuka kutokana na mtikisiko wa uchumi
duniani, bado iliendelea kupanda kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo kati ya
2010 na 2011.
Akizungumzia soko la maji ya Serengeti
ukilinganisha na soko hilo kwa nchi jirani kwa kuzingatia itifaki ya soko la
forodha la EAC hasa kwa wazawa, Mathayo anasema kwa sasa hali ya soko ni nzuri
tofauti na hapo awali kwani kwa sasa ulipaji wa ushuru upo sawa na wanaoingiza
ambapo zamani bidhaa toka nje ya nchi hazikuwa zinalipiwa ushuru hivyo
wawekezaji wa ndani hawakupata faida nzuri na soko lilikuwa kidogo tofauti na
hivi sasa.
“ Hatua hii imetusaidia kukabiliana na ushindani
wa soko kwa kuwa wawekezaji wa nje sasa wanalazimika kulipa ushuru kwenye nchi
zao na kulipa tena wanapoingiza bidhaa hizo hapa nchini kwetu, hivyo kwa
kufanya hivyo wamejikuta wakiiongiza bidhaa mbalimbali yakiwemo maji kwa
kiwango kidogo kutokana na kulipa ushuru mara mbili na kutuachia nafasi kubwa
la soko” anasema.
Anaelezea tofauti ya uzalishaji ulivyokuwa wakati
maji ya kiwanda hicho yakiitwa Super na sasa yanapoitwa Serengeti kwamba
uzalishaji kipindi kile ulikuwa mkubwa sana lakini soko halikuwepo tofauti na
kipindi hiki ambapo uzalishaji umepungua lakini soko liko juu sana
ukilinganishwa na hapo zamani.
Anaeleza sababu za kushuka kwa kiwango cha
uzalishaji wa maji kiwandani umetokana na kupungua kwa nguvu ya mitambo
iliyotengenezwa nchini China na sasa wanampango wa kuagiza mitambo mipya toka
nchini India ambayo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha maji hivyo hatua hiyo
itaongeza kukua kwa soko la maji ya Serengeti kwa ndani na nje ya nchi.
Mathayo anasema maji hayo wakati yakiitwa Super
Water kiwanda kilizalisha wastani wa lita 1500 kwa saa lakini hali ni tofauti
kawa sasa amapo uzalishaji ni wastani wa kati lita 600 hadi 800 kwa saa huku
mpango wa kiwanda ukiwa ni kuagiza mitambo itakayozalisha lita 5000 kwa saa
moja.
Kwa upande mwingine Mathayo anaeleza sababu za
kiwanda chake kutumia maji ya visima kuzalisha na kusindika maji ya Serengeti
badala ya maji ya Ziwa Victoria na anasema mtazamo wa watumiaji wengi ni kwamba
maji ya ziwa ni maji machafu yenye mizoga na hayafai kunyweka na kwa msingi huo
waliona watumie maji ya chanzo chao kikuu ambacho ni kisima kirefu cha
kuchimbwa japo ukweli ni kwamba maji ya ziwa ni safi na hayana chumvi kama
wengi wanavyodai.
Anatoa mfano hai wa maji ya Ruwenzori ya nchini
Uganda kwamba yanatokana na maji ya Ziwa lakini kwa sababu yanaingizwa ndani ya
nchi yetu wananchi na ambao ndiyo wateja wa bidhaa ya maji hawawezi kufuatilia
na kuzingatia sana suala hilo kwa kuwa yanatoka nchini Uganda lakini ukweli ni
kwamba hayatoki mlima Ruwenzori kama wanavyodhani watu wengi.
Baadhi ya watalii waliotembelea hifadhi ya
wanyama ya Serengeti hivi karibuni kabla ya kuondoka kurudi kwao nchini
Hispania wanaeelezea jinsi gani walivyofurahishwa na utalii wao ndani ya
hifadhi kwa kuwaona wanyama wa aina mbalimbali lakini pia huku wakiburudika kwa
maji na bia ya Serengeti.
Mmoja wa kundi la watalii hao Sara Alza Puravuda
na Patricia Ponce Mateos toka Majiji ya Barcelona na Sevilla nchini Hispania
wanasema kwa muda wote waliokuwa wakifanya utalii ndani ya hifadhi ya Serengeti
walipata fursa ya kukutana na bidhaa hizo zenye jina sawa na hifadhi
waliyokuwemo na kuelezea kwamba hatua hiyo itazidi kulipaisha jina la Serengeti
katika vivutio maalum vya utalii kimataifa hivyo kuisaidia Tanzania kuongeza
idadi kubwa ya watalii.
MWISHO.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mara Dairy James Mathayo akitoa maelezo ya usindikaji wa maji ya Serengeti kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe katika moja ya maonesho ya kibiashara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni