Ijumaa, 23 Januari 2015

WAZIRI KABAKA KUONGOZA MAELFU YA WASABATO KAMUNYONGE






                                                   Pichani: Mhe Gaudensia Kabaka.




Waziri wa Kazi na Ajira Mhe:Gaudensia Kabaka January 25 mwaka huu anatarajia kuongoza maelfu ya waumini wa  kanisa la Waadventista la Wasabato la Kamunyonge la Musoma Mjini  ambalo ni kanisa Kuu la Wasabato jimbo la Mara, katika sherehe maalum ya kwaya ya kanisa hilo (Choir day) itakayofanyika katika viwanja vya kanisa hilo.



Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kanisa hilo la Wasabato la Kamunyonge bw. Bigambo Jeje amesema kuwa mbali na Waziri Kabaka baadhi ya viongozi wengine wa serikali akiwemo Mkuu wa mkoa wa Mara Kepteni mstaafu Aseri Msangi,Katibu Tawala wa mkoa wa Mara Benedct Ole Kuyan sanjari na wakuu wa wilaya za Musoma,Bunda na Butiama, Jackson Msome, Joshua Mirumbe na Anjelina Mabula wamealikwa katika sherehe hiyo.


Bw. Jeje amesema kuwa viongozi wengine mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa,mashirika ya umma,wakuu wa idara za serikali,wafanyabiashara  sambamba na viongozi wa madhehebu ya dini wamethibitisha kushiriki katika sherehe hizo zitakazoenda sanjari na uzinduzi wa kanda za nyimbo za Video na Sauti za kwaya hiyo kongwe hapa nchini.


Amefafanua kwamba lengo la harambee hiyo ni kupsta fedha zisizopungua milioni 50 zitakazotumika kwa ajili yamiradi ya maendeleo ya kwaya hivyo kuisaidia kwaya hiyo kujikwamua kiuchumi na kuachana na utegemezi wa wahisani mbalimbali pindi inapokuwa ikihitaji kutekeleza majukumu yake.


Ametanabaisha kuwa hii itakuwa ni harambee ya pili ya kwaya kufanyika harambee katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo katika harambee ya kwanza ya Septemba 04 mwaka 2010,Rais Jakaya Kikwete alichangia kiasi cha sh.milioni 3 na kufanikisha kupatikana kwa jumla ya sh milioni 12 zilizotumika katika shughuli mbalimbali za kwaya hiyo.


Aidha Mkurugenzi huyo wa Mawasiliano katika kanisa hilo amesema baada ya kumalizika kwa harambee hiyo,kwaya itakuwa katika maandalizi ya mwisho kwa ajili ya safari yao ya kwenda jijini Dar es Salaam huku wakiliwakilisha jimbo la Mara katika mkutano mkubwa wa injili wa kimataifa unaozishirikisha nchi 11 za Afrika Mashariki,Kati na Pembe ya Afrika utakaoanza February mosi mwaka huu na kufunguliwa rasmi na Rais Kikwete uwanja wa Taifa siku tatu baadaye mnamo February 4.


MWISHO.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni