Bigambo Jeje,Musoma
Wananchi zaidi ya 4000 wa vijiji vitatu
vya kata ya Busambara katika halmshauri ya wilaya ya Musoma Vijijini mkoani
Mara watanufaika na huduma za afya baada ya zahanati inayojengwa katika kijiji
cha Mwiringo kwa gharama y ash. milioni 150 kukamilika siku chache zijazo.
Mganga mkuu wa halmashauri hiyo ya
Musoma Vijijini Dk Genchwere Makenge amewaambia waandishi wa habari mjini
Musoma kuwa ujenzi huo unaofadhiliwa na wafadhili mbalimbali akiwemo bw.
Michael Mujinja unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi January mwaka huu na
kupisha huduma za afya kuanza mara moja.
Dk Makenge amesema kukamilika kwa
zahanati hiyo ya kisasa ya kijiji cha Mwiringo kutapunguza adha ya wananchi wa
vijiji vya kata hiyo vya Kwikuba,Busambara na Mwiringo waliokuwa wakipata
huduma za afya katika kata ya jirani ya Mugango na wakati mwingine kulazimika
kwenda hospitali ya serikali ya mkoa wa Mara iliyopo mini Musoma.
Ametanabaisha kuwa awali ujenzi huo ulikumbana
na changamoto kadhaa zikiwa ni pamoja na wananchi kusuasua kuchangia nguvu zao
za kujitolea kusoma mawe,matofali,maji na mchanga wakidhani kuwa jukumu hilo
lilikuwa la wafadhili pekee lakini walishiriki kikamilifu baada ya kuhamasishwa
na kufahamu kuwa mradi huo ulikuwa si kwa faida ya mtu mwingine bali jamii yao
kwa ujumla.
Amesema sababu za kisiasa nazo
zilichangia kuzorota kwa ujenzi wa zahanati hiyo ambapo baadhi ya wanasiasa
walipita huku na kule wakiwapotosha wananchi kuwa mradi huo ulikuwa ni wa watu
binafsi na si wa serikali jambo lililosababisha wengi wao kukatishwa tama hadi
hapo uongozi wa halmshauri ulipoishirikisha jamii na hatimaye mwanakijiji mmoja
bw. Merika Rwoti akakubali kutoa shamba lake bila shuruti ili ujenzi uanze.
Akizungumzia miradi mingine ya afya
katika halmshauri hiyo ya Musoma, Dk Makenge amesema kuna vijiji 68 lakini kati
ya hivyo vyenye zahanati ni 27,hivyo kuwa na upungufu mkubwa wa zahanati kwa
mujibu wa sera ya afya ya kusogeza karibu huduma za afya kwa kila kata kuwa na kituo cha afya sanjari
na kila kijiji kuwa na zahanati.
Mganga mkuu huyo amefafanua kuwa ujenzi
wa zahanati katika kata za Etaro na Kigera Etuma ama umekamilika au uko
katika hatua za mwisho huku ujenzi wa zahanati za Chirorwe na Maneke ukiendelea kwa hatua ya kati wakati ujenzi
huo kwa zahanati ya kijiji cha Nyasaungu ukiwa katika hatua ya awali.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni