Na Bigambo Jeje,Musoma.
Waziri wa Kazi na Ajira Mhe:Gaudensia Kabaka amewataka viongozi wa
madhehebu ya dini kubuni miradi ya maendeleo katika taasisi za kidini
wanazoziongoza ili kusaidia kupatikana kwa ajira katika sekta binafsi sanjari
na kupunguza umasikini uliokithiri katika jamii hivyo kuisaidia serikali
kutekeleza kwa vitendo dira ya taifa ya maendeleo.
Waziri Kabaka ametoa kauli hiyo jana katika hotuba iliyosomwa kwa
niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Bunda mkoani Mara Joshua Mirumbe wakati wa
sherehe maalum ya kwaya iliyoambatana na harambee ya kuchangia fedha za miradi
ya maendeleo ya kwaya ya kanisa la Wasabato la Kamunyonge la Mjini Musoma
iliyofanyika katika viwanja vya kanisa hilo.
Amesema kuwa madhehebu ya dini yanayo nafasi kubwa ya kuhakikisha
kwamba yanaanzisha miradi itakayowasaidia waumini wao kupata ajira hivyo licha
ya waumini kujipatia kipato bali pia taasisi hizo za kidini zitajiimarisha
kiuchumi kwa kupata matoleo ya sadaka na zaka za uhakika na kuendesha shughuli
zao bila kutegemea misaada ya wahisani wa ndani na nje ya nchi.
Amewataka viongozi wote wa madhehebu ya dini hapa nchini kujikita
zaidi katika miradi ya kiuchumi,elimu na afya kwa kuanzisha vikundi vya kuweka
na kukopa,shule za msingi,sekondari na vyuo mbalimbali sambamba na miradi ya
afya kama vile zahanati,vituo vya afya na hospitali, hatua itakayoleta
matumaini makubwa kwa wananchi wanaoishi katika hali ya umasikini mkubwa.
Waziri Kabaka katika harambee hiyo alichangia kiasi cha sh milioni
3 huku mkuu wa wilaya ya Bunda akichanga sh laki saba kati ya kiasi cha sh
milioni 15 zilizopatikana zikiwa ni taslimu na ahadi kutoka kwa waalikwa
mbalimbali waliohudhuria katika harambee iliyoendana pia na uzinduzi wa kanda
za nyimbo za Video na Sauti za kwaya hiyo kongwe hapa nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa kwaya hiyo Asheri Mukama amesema lengo la
harambee hiyo ilikuwa ni kupata fedha kiasi cha sh milioni 50 zinazohitajika
kwa ajili yamiradi ya maendeleo ya kwaya hivyo itakayosaidia kwaya kujikwamua
kiuchumi na kuachana na utegemezi wa wahisani mbalimbali pale inapokuwa
ikihitaji kutekeleza majukumu yake.
Mukama amefafanua kuwa hiyo ni harambee ya pili ya kwaya kufanyika
tangu Septemba 04 mwaka 2010,wakati Rais Jakaya Kikwete alipochangia kiasi cha
sh.milioni 3 na kufanikisha kupatikana kwa jumla ya sh milioni 12 zilizotumika
katika shughuli mbalimbali za kwaya hiyo.
Aidha amesema baada ya kumalizika kwa harambee hiyo,kwaya
inajiandaa kwa safari yao ya kwenda jijini Dar es Salaam kuliwakilisha kanisa
la Wasabato jimbo la Mara katika mkutano mkubwa wa injili wa kimataifa
unaozishirikisha nchi 11 za Afrika Mashariki,Kati na Pembe ya Afrika utakaoanza
February mosi mwaka.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni