Na Bigambo Jeje
Hatimaye swahiba zamani wa karibu
kisiasa wa mgombea urais wa UKAWA Edward Lowassa, Vedastus Mathayo amevunja ukimya
na kuutangazia umma kwamba yeye na Lowassa urafiki wao kisiasa ulikoma tu pale
alipohama CCM na kwenda CHADEMA.
Aidha amekanusha uvumi uliokuwa umetanda
kwamba angeweza kuhamia CHADEMA kumfuata Lowassa kutokana na ukaribu wa kisiasa
waliokuwa nao hususani katika kinyang’anyiro cha kura ya maoni ya Urais wa CCM
na badala yake akawataka wana Mara na Watanzania kwa ujumla kumchagua Mgombea
Urais wa CCM Dk John Magufuli.
Mathayo alitoa kauli hiyo jana katika
mkutano wa huo wa hadhara wa chama hicho uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya
Msingi Mukendo na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi waliohudhuria kumsikiliza
mgombea ubunge huyo kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Musoma Mjini huku
akitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kwa kumpa kura za kimbunga wakati wa
kura ya maoni ambapo aliibuka kidedea kwa zaidi ya asilimia 75.
“ Watu walizusha kuwa mimi nahamia
CHADEMA eti kwa sababu Lowassa ni rafiki yangu lakini nataka niweke wazi na
kuwaondoa hofu kuwa nitabaki CCM na kamwe siwezi kumfuata Lowassa maana kila
mtu aliingia CCM tarehe,siku,mwezi na mwaka tofauti hivyo kuondoka kwake ni
utashi wake binafsi usionihusu hata kidogo” na kuongeza kuwa
“ Ila atakapokuja Musoma nikiwepo
nitaenda kumsalimia kwa kuwa mahusiano yaliyobaki ni ya kibinafsi kwa vile
urafiki kwa mtu yeyote yule hauwezi kutengwa na harakati za kisiasa lakini
kuanzia sasa nitasimama popote pale kuomba na kutafuta kura za Urais za
Magufuli ambaye ni mgombea wa chama changu”.
Mgombea ubunge huyo alisikitishwa na
hali ya kushuka kwa kiwango cha elimu katika Manispaa ya Musoma kutokana na
changamoto kadha wa kadha ukiwemo upungufu wa madawati na usimamizi mbovu wa
halmashauri inayoongozwa na madiwani wengi wa CHADEMA.
Kwa msingi huo alisema hata kabla ya
kupewa ridhaa ya kuingia madarakani hapo Oktoba 25 mwaka huu,Chama cha
Mapinduzi kitatoa madawati 13,932 yenye thamani ya zaidi ya sh milioni 905 ili
kuondoa tatizo la madawati katika shule za msingi.
Kwa upande wa shule za sekondari alisema
amejiandaa kupambana na matokeo ya kidato cha nne ambayo kila mwaka katika
Manispaa ya Musoma yanazidi kushuka huku idadi ya wanafunzi wanaopata divisheni
sifuri ikifikia 500 kati ya wahitimu wapatao 1100 waliohitimu katika shule hizo
hapo mwaka jana.
Akizungumzia suala afya alisema kama
wananchi wataipa ridhaa CCM ikashika dola katika Manispaa ya Musoma
watahakikisha zahanati na vituo vya afya vilivyopo vinaboreshwa kwa kuongeza
vifaa tiba na kusimamia sera ya serikali kwa kutoa huduma bure kwa
wajawzito,watoto chini ya umri wa miaka mitano na wazee wenye umri wa zaidi ya
miaka 70 wakati wazee wa kawaida akiahidi kuwasaidia kuwasajili katika mpango
wa bima ya afya.
Aliishukuru serikali kuendelea
kutekeleza ahadi yake ya umaliziaji wa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Kwangwa
kama Rais Jakaya Kikwete alivyoahidi Septemba 25 mwaka 2010 wakati akiomba
ridhaa ya wananchi wa Musoma Mjini wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita
ambapo hadi sasa serikali imeshatoa zaidi y ash bilioni 2 kuendelea na huo
ujenzi.
Mathayo alisema kabla ya kumalizika kwa
ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Kwangwa, atafanya utaratibu wa kuwasaidia gari
na mafuta, wagonjwa wanaotoka familia maskini watakaopewa rufaa ya kwenda
Bugando jijini Mwanza ili kuokoa maisha yao tofauti na sasa ambapo wengi
wanakoswa fursa hiyo kutokana na ama uongozi wa hospitali kutokuwa na ruzuku ya
kutatua tatizo hilo au viongozi wa sasa wa halmshauri ya Manispaa toka CHADEMA
kutokuwa na moyo wa kujali na kuthamini wananchi wao waliowaweka madarakani.
Kuhusu suala la mapambano ya vita dhidi
ya umasikini, Mjumbe huyo wa NEC ameahidi kutoa sh milioni 200 kwa ajili ya
kuwasaidia wanawake kupata mikopo nafuu isiyo na riba kupitia vikundi vyao vya
ujasiriamali, mikopo kwa vijana sanjari na kuanzisha makambi ya kupata mafunzo
ya kujitegemea atakayoyafadhili yeye huku wazee nao wakiahidiwa kupewa mikopo
kupitia Umoja wao wa Wazee wa Musoma Mjini.
MWISHO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni