Jumanne, 2 Agosti 2016

MAKUSANYO YA NDANI YANUFAISHA MJI WA MUSOMA MARA MBILI



WATU waliowahi kuishi Musoma mjini, mkoani Mara miaka ya themanini hadi tisini na kisha kuondoka, bila shaka wana kumbukumbu ya mji uliokuwa msafi, ukiwa na barabara zisizotuamisha maji hata kama ni masika na barabara zenyewe ni za vumbi.

Katika miaka ya karibuni, mji wa Musoma umebadilika, hatua ambayo bila shaka inasababishwa pia na ongezeko la watu na matumizi makubwa ya ardhi kwa ajili ya uchumi wa wakazi wa mji huo.

 Katika harakati za kurejesha hadhi ya mji wa Musoma kwa maana ya usafi wa mazingira na miundombinu bora, Benki ya Dunia (WB) imetoa mkopo wenye masharti nafuu wa zaidi ya Sh bilioni 3 ili kujenga barabara ya kiwango cha lami katika Manispaa ya Musoma.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Dk Khalfan Haule anasema kutolewa kwa fedha hizo kumetokana na kutimiza masharti ya benki hiyo iliyoyatoa ikiwa ni pamoja na kutaka kuona juhudi zaidi za halmashauri hiyo katika kukusanya mapato yake ya ndani.

 Ni kwa hatua hiyo anasema halmashauri imepata faida mara mbili. Haule anasema fedha hizo zimetumika kujenga barabara ya kiwango cha lami toka kituo cha afya cha Nyasho hadi barabara ya Majita kupitia eneo la Kamunyonge.

Barabara hiyo ina urefu wa kilometa 2.5. Anasema kwa sasa ujenzi unaendelea chini ya mkandarasi ambaye ni kampuni ya Ujenzi ya Nyanza ya jijini Mwanza iliyoanza kazi hiyo mwanzoni mwa mwaka wa fedha wa 2015/16 na unatarajia kukamilika miezi michache ijayo.

Anasema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kwa viwango vilivyowekwa na benki hiyo ya dunia, utafungua nafasi kwa halmashauri hiyo ya Manispaa ya Musoma kuendelea kupata mikopo mingine zaidi kwa ajili ya ujenzi wa baadhi ya barabara nyingine zenye urefu wa kilometa 10 kwa kiwango cha lami pia.

“Naweza nikasema kwamba tupo kwenye hatua za mwisho za mazungumzo na wafadhili wetu hao ili watusaidie fedha zitakazotumika kujenga barabara nyingine ndani ya Manispaa yetu, hivyo kuimarisha miundombinu itakayowezesha mji kuwa katika hali ya unadhifu na usafi wa mazingira,” anafafanua.

Anaongeza: “Hii ni faraja kubwa sana kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma wapatao 150,000 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kwa kupata barabara za lami ambazo zinaufanya mji kuwa na miundombinu bora na ya kudumu, hivyo kuwa chachu ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi.” 

Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Musoma anasema anataka kuirejesha historia ya usafi wa mazingira ya miaka ya tisini ambayo iliifanya Musoma kushika nafasi ya kwanza hapa nchini kwa miaka mitatu mfululizo.

Anasema hatua hiyo ilifikiwa kutokana na usafi wa mazingira na miundombinu yake, kulinganisha na majiji, manispaa, miji na halmshauri zote za Tanzania. Anafafanua kwamba hiyo ilikuwa mwaka 1992, 1993 na 1994 wakati Halmashauri ya Mji wa Musoma kwa wakati huo ilipoongoza kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo na kujiletea heshima kubwa kitaifa na kimataifa na kuyafanya baadhi ya majiji duniani kutoa tuzo maalumu za kuipongeza kwa hatua hiyo ya kuongoza katika suala zima la usafi wa mazingira.

Dk Haule anasema wakati huo, halmashauri iliyokuwa chini ya aliyekuwa Meya wa Mji, Eliasafu Masige Lima na kwamba mikakati kadha wa kadha iliwekwa ikiwa ni pamoja na ushirikiano mkubwa baina ya watumishi wa afya na wananchi.

Anasema mara ya mwisho kwa mji huo kufanya vizuri katika usafi ni mwaka 2002. Anaitaja mikakati iliyoleta mafanikio katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na kutolewa kwa elimu katika jamii ya wakazi wa kata zote za mji, kuwepo nguvu kazi ya ziada ya vibarua kwenye idara ya afya iliyofanikisha kwa kiasi kikubwa na vibarua hao walikuwa wakilipwa na ofisi ya Mkurugenzi sanjari na usimamizi mzuri kwenye ngazi ya kata.

Mikakati mingine inayotajwa iliyotumika kuiletea sifa Manispaa ya Musoma na kufikia kuwa kinara wa usafi wa mazingira kuliko halmashauri zote nchini ni uwepo wa vifaa vya kufanyia usafi ikiwa ni pamoja na magari ya maji machafu na taka ngumu huku sheria ndogo ndogo za halmshauri zikitumika kuwasimamia wananchi.

“Kama Manispaa tumeamua kwa dhamira ya dhati kutumia miradi ya barabara katika Manispaa yetu kuwa chachu kubwa ya wananchi kukuza uchumi na kujiletea maendeleo lakini pia tunaamini itachangia kurejesha historia ya kuwa vinara wa usafi nchini,” anasema.

 “Kama wenzetu chini ya Mzee Eliasafu Lima waliwejiwekea mikakati na wakafanikiwa kuiweka Musoma kwenye ramani ya kitaifa na kimataifa, basi ni dhahiri kuwa na sisi hatuna sababu ya kushindwa kuyafikia mafanikio hayo,” anasema.

Mkurugenzi Haule anasema mbali na mradi wa Benki ya Dunia, halmashauri hiyo pia imefanikiwa kutekeleza miradi mingine ya barabara katika kata mbalimbali katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha wa 2015/16 inayoanzia kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu. Anasema barabara hizo zinapitika licha ya changamoto ya mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha.

Anasema kwamba katika kipindi hicho cha robo ya tatu na kwa kutumia fedha za mfuko wa barabara zipatazo milioni 149.7 kazi nyingi zimefanyika katika kuimarisha miundombinu ikiwemo kufanya matengenezo ya kawaida katika barabara za Nyamatare, Kigera na Mutex. Halikadhalika anasema wameziba viraka vya lami katika barabara za Kamunyonge, Mukendo na Iringo.

“Tayari makandarasi wamekamilisha kazi katika barabara za Nyamatare kilometa 3 kwa kujenga kalvati 1 kwa Sh milioni 4.7, Kigera kilometa 3 kwa kujenga kalvati 1 kwa Sh milioni 8.4, Mutex - Buhare wamejenga nguzo za hifadhi ya barabara 90 kwa sh milioni 16.2 huku barabara ya Kamunyonge yenye kilometa 3 ikijengewa kalvati moja kwa thamani ya Sh milioni 7.3,” anasema.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma anaeleza hatua zilizochukuliwa na halmashauri yake katika mapambano ya wananchi juu ya umasikini kupitia mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ambapo jumla ya Sh bilioni 3.02 zimetumika hadi kufikia robo ya tatu ya kati ya Januari na Machi mwaka huu katika kusaidia kaya masikini.

Dk Haule anasema lengo la mradi huo wa Tasaf kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 ni kutambua, kuandikisha, kuhakiki na kulipa ruzuku kwa kaya masikini na tayari ruzuku imetolewa kwa kaya 2707 zilizojitokeza siku ya malipo kwa awamu ya nne ya malipo hayo huku kiwango cha umasikini kwa walengwa kikiwa kimepungua kwa kiwango cha kati.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni