Jumapili, 21 Agosti 2016

MUSOMA EXPRESS NA CATA MINING ZATOA MISAADA YA SH BILIONI 1.2 MUSOMA

Na Bigambo Jeje,Musoma.
Agosti 3 2016.
MISAADA.

Pichani ni moja ya Mabasi mapya 18 ya kampuni ya Mabasi ya Musoma Express yanayotoa huduma za usafiri katika mikoa mbalimbali ya hapa nchini. 

Makampuni ya mabasi ya Musoma Express na Mgodi wa madini wa CATA uliopo wilaya ya Butiama mkoani Mara yametoa misaada ya zaidi ya sh bilioni 1.2 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kusaidia shughuli za maendeleo ya kijamii katika sekta mbalimbali kwa lengo la kupunguza umasikini na kukuza uchumi wa wananchi.


Kutolewa kwa misaada hiyo ya kijamii katika sekta mbalimbali za elimu,maji,barabara na miundo mbinu kwa wananchi wa mkoa wa Mara ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya uwekezaji ya Taifa inayowataka wawekezaji kutoa sehemu ya mapato yao kusaidia huduma za kijamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa makampuni hayo ya mabasi ya Musoma Express na mgodi wa CATA Bw. Mauza Nyakirang’anyi amesema misaada hiyo imetolewa kwa wananchi wa vijiji kadhaa vya  halmashauri za wilaya za Musoma Vijijini na Butiama kama mchango wa makampuni hayo katika kusukuma mbele  gurudumu la maendeleo ya wananchi ili kujikwamua kwenye umasikini.
 
Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu huo, makampuni yake yametoa sh bilioni 1.1  kwa ajili ya ujenzi wa barabara mpya ya kutoka kijiji cha Kataryo kupitia Kyawazaru hadi vijiji vya Nyakiswa,Nyamikoma hadi Kukirango yenye urefu wa km 7 iliyogharimu sh milioni  500 huku sh milioni 600 zikitumika kwenye ujenzi wa madaraja  makubwa mawili kwenye mto Kyarano kwenye halmshauri hizo mbili.

Ameitaja misaada mingine kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya shule ya sekondari ya Kukirango uliogharimu sh milioni 11.5, mchango wa sh milioni 7.8 kwenye ujenzi wa miundo mbinu ya kuweka umeme katika shule ya sekondari Tegeruka sanjari na msaada wa sh milioni 2 za ukarabati wa madarasa mawili ya shule ya msingi Kwawazaru.

Bw. Mauza amesema kwamba makampuni yake pia yametumia zaidi ya sh milioni 60  katika zoezi la uchimbaji wa visima vitano vya maji sambamba na uchangiaji ujenzi wa shule ya sekondari ya Kiabakari na kuongeza kuwa makampuni hayo ya Musoma Express na mgodi wa CATA kwa pamoja yataendelea kutoa huduma za kijamii za wananchi walio katika lindi la umasikini.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo Mtendaji amezishukuru benki za CRDB na ile ya Maendeleo ya TIB kuwezesha gharama za uwekezaji wa ujenzi wa mgodi wa CATA baada ya kutoa mkopo wenye riba nafuu wa dola za Kimarekani  milioni 54 ambazo ni zaidi ya sh bilioni 108 na kuzitaka benki nyingine kuiga mfano huo kwa kuwa mstari wa mbele kuwezesha wawekezaji wazawa.

MWISHO.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni