WANAWAKE
katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara wamepata mikopo yenye thamani ya Sh
milioni 200 itakayowasaidia katika shughuli za kiuchumi kupitia ujasiriamali.
Mikopo
hiyo yenye riba nafuu imetolewa na Mbunge wa Musoma Mjini mkoani Mara kupitia
tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Vedastus Mathayo, ikiwa ni utekelezaji wa
moja ya ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa
Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Wakati
wa kampeni hizo, mwanasiasa huyo aliahidi kutoa shilingi milioni 200 kwa ajili
ya kuwasaidia wanawake na milioni 50 za kuwawezesha vijana kiuchumi.
“Nimeanza
utekelezaji wa ahadi zangu na hili suala la mikopo kwa akinamama wa daraja la
chini nimelikamilisha kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu kuelekea
uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka jana na ndiyo maana nimetoa milioni 200
kuwasaidia wanawake katika shughuli za ujasiriamali,” anasema Mathayo.
“Katikati
ya mwezi huu wa Januari mtakumbuka nilizungumza na wenyeviti wa mitaa 73 ya
Jimbo la Musoma Mjini na kuwapa jukumu la kusajili vikundi vya wanawake
watakaowezeshwa fedha hizo. Nawapongeza kwa kuitikia mara moja zoezi hilo na
tayari wanawake wameanza kupokea mikopo yao ya Sh 250,000 kwa kila kikundi cha
watu 5 huku wakitakiwa kurejesha mikopo yao kwa riba ya asilimia mbili tu,”
anasema.
Anasema,
wakati anatoa ahadi hiyo ilikuwa si kutafuta kura pekee, alikuwa na dhamira ya
kuwasaidia wananchi kupitia shughuli zao za ujasiriamali ili waweze kuwa na
uchumi bora na kuondokana na umasikini unaowakabili kutokana na sababu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji.
Mathayo
anasema, hahitaji kurudishiwa fedha hizo, ziwe na mpango mzuri ambao utaweza
kuwawezesha wananchi kuzitumia kwa lengo la kuongeza kipato kwa kufanya
ujasiriamali na si kuzitumia kwa njia isiyofaa.
Anasema,
mikopo hiyo itakuwa inarejeshwa kwa lengo la kuwawezesha wanawake ambao
hawajapata fursa hiyo nao waweze kukopeshwa. “Nimetoa fedha hizi kama ruzuku
katika kuwasaidia wananchi wangu wa Jimbo la Musoma mjini, niliahidi na
nimetekeleza na kinachohitajika ni usimamizi kuona fedha hizi zinatumika
kuwasaidia na watu walioteuliwa kufanya zoezi la utoaji wa fedha wahakikishe
fedha zinapotolewa ziende zikafanye kazi za kujenga uchumi,” anasema Mathayo.
Mbunge
huyo anasema amekubaliana na uongozi wa benki Kata ya Imara (SACCOS) iliyopo
Musoma Mjini kwa kushirikiana na watu wawili aliowateua kuweza kuweka mipango
endelevu itakayoweza kuwasimamia wananchi kuzitumia fedha hizo kwa kuinua
kiwango chao kiuchumi.
Mwenyekiti wa Benki Kata hiyo, Boniphace Ndengo anasema
wanachokifanya sasa ni utoaji wa elimu ya ujasiriamali kwa wananchi kabla ya
kuwakabidhi fedha.
Anasema,
lengo la elimu hiyo ni kuwaandaa kisaikolojia kuhusu umuhimu wa kukopa na jinsi
ya kurejesha mikopo yao kwa wakati sambamba na jinsi ya kuitumia kwa malengo
yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
Ndengo
anasema, umewekwa utaratibu wa kurahisisha upatikanaji wa fedha hizo kupitia
wenyeviti wa mitaa hivyo wanawake wafike kwenye ofisi za serikali za mitaa na
kuanza taratibu za kujiunga kwenye vikundi.
Mkazi
wa kata ya Nyasho, Kulwa Biseko ni miongoni mwa wanawake ambao tayari
wamenufaika na mikopo hiyo waliyoichukua wiki iliyopita.
Anamshukuru
Mbunge Mathayo kwa kutekeleza ahadi yake kwa haraka na kutekeleza kwa vitendo
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010-2015. Ibara ya 76 ya Ilani hiyo inaielekeza
serikali kufufua kwa nguvu zote elimu yenye manufaa ya watu wazima nchini kote
ili masomo ya ujasiriamali, uwezeshaji, urasimishaji wa biashara, kilimo,
ufugaji na uvuvi yaweze kutolewa kwa wananchi wengi.
“Moja
ya sehemu ya ibara hiyo inazungumzia umuhimu wa elimu kutolewa kwa njia ya
mafunzo yanayolenga katika kuutokomeza umasikini wa wananchi walio wengi. Hivyo
mafunzo ya ujasiriamali tuliyopewa kabla ya kupata mikopo hii ni sehemu ya utekelezaji
wa Ilani ya CCM na tunampongeza kwa dhati Mbunge wetu kuanza uongozi wake kwa
kutekeleza falsafa ya Rais Magufuli ya Hapa ni Kazi Tu,” anasema Biseko.
Anaiomba
serikali kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 -2020
kwa kuliangalia kundi kubwa la masikini lililo katika maisha ya chini kama
ilivyobainishwa katika ibara ya 76 (b) kwa kuhamasisha uanzishwaji wa ushirika
wa kuweka na kukopa (SACCOS na VICOBA), wa mazao, ujenzi, uvuvi, biashara na
aina nyingine za ushirika ili wananchi wengi zaidi wajiunge na ushirika na
wawezeshwe kimtaji kupanua shughuli zao za uzalishaji mali.
Anatoa
mwito kwa viongozi wengine kuiga mfano wa Mbunge Mathayo aliyetoa fedha kutoka
kwenye kipato chake na kuwasaidia wanawake Musoma Mjini wajikomboe kiuchumi.
Anaiomba Serikali ya Awamu ya Tano kukuza mifuko ya uwezeshaji, kuboresha
usimamizi na taratibu za kutoa mikopo ya riba nafuu ili walengwa wengi zaidi
waweze kunufaika.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni