Jumatano, 3 Agosti 2016

MUSOMA KUMALIZA TATIZO LA MAJI KWA VIWANDA, WAWEKEZAJI




Imeandikwa na Bigambo Jeje
Imechapishwa: 03 Agosti 2016


MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa) mkoani Mara inatarajia kuanza kuzalisha lita milioni 36 za maji kwa siku ifikapo Sepetemba mwaka huu hivyo kuwa na ziada ya lita milioni 12 za maji kila siku.

Hali hiyo inaipa uhakika wa huduma hiyo kwa wawekezaji mbalimbali wenye mahitaji makubwa ya maji. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Muwasa, Said Gantala anasema hatua hiyo sasa itasaidia kuvutia wawekezaji mbalimbali, wakiwemo wale wa viwanda vikubwa na vidogo vya nguo, usindikaji wa samaki, mbogamboga, maziwa na matunda sanjari na bidhaa za aina tofauti za vyakula kuja kuwekeza katika Manispaa ya Musoma na kusaidia kukuza pato na uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Gantala alitoa taarifa hiyo njema Julai 30 mwaka huu wakati wa akiongoza mamia ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo kufanya usafi kwenye mradi mkubwa wa maji wa Bukanga ambao ujenzi wake unaelekea hatua za mwisho.

Gantala anasema kama ilivyo kwa taasisi na mashirika mengine ya umma, suala la usafi wa mazingira limekuwa likifanywa na mamlaka hiyo mara zote ikizingatiwa aina ya huduma inayotolewa na Muwasa ya kusambaza maji kwa wananchi kuwa inatakiwa kuzingatia vigezo vyote vya usafi, licha ya kutekeleza pia agizo la Rais John Magufuli la kufanyika kwa usafi kila mwisho wa mwezi.

Anasema kwa muda wa miaka mingi, Manispaa ya Musoma imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa za kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya kiuchumi na tatizo la maji likiwa ni miongoni mwa changamoto hizo. Lakini anasema katika kipindi cha mwezi mmoja ujao kero ya upungufu wa maji itakuwa historia katika manispaa hiyo.

“Tumekuwa na viwanda kama cha nguo cha Mutex ambacho ni kiwanda kikubwa cha nguo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati sambamba na kiwanda kikubwa kingine cha kusindika minofu ya samaki cha Prime Catch kilichopo Bukanga lakini vimekuwa vikishindwa kupata maji ya kutosha na yenye uhakika kutoka Muwasa, lakini kuanzia mwezi ujao tatizo hilo litakwisha,” anasema.

Anatanabaisha kwamba Muwasa kwa muda wa miaka mingi imekuwa ikizalisha lita zipatazo milioni 10 kwa siku huku mahitaji yakiwa ni milioni 24, jambo linalosababisha kuwepo kwa upungufu wa lita milioni 14 kila siku na hivyo kushindwa kukidhi mahitaji makubwa ya viwanda na miradi mingine mikubwa yenye kujiendesha kwa kutegemea huduma ya maji. Mradi wa maji wa Bukanga unajengwa kwa gharama ya Sh bilioni 45 na utakuwa ukiwahudumia wakazi wapatao laki moja na nusu wa Manispaa ya Musoma.

Katika hatua nyingine, Gantala anasema ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wa kata za pembezoni mwa Manispaa ya Musoma, tayari ujenzi wa tangi la maji litakalotumika kusambaza maji katika kata za Rwamlimi na Bweri umekamilika. Tangi hilo limejengwa kwa nguvu za Muwasa katika kutekeleza mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) ambapo mamlaka hiyo inatarajia kuongeza wateja 1,000 kupitia tangi hilo.

Mkurugenzi huyo wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma anasema tangi hilo lina ujazo wa kita 135,000 na litahudumia maeneo ya Rwamlimi, Songambele, Songe na taasisi nne za shule za sekondari. Pia anasema litatumika kama tangi saidizi (Break Pressure Tank) la tangi kuu litakalojengwa kilima cha Kwangwa.

“Gharama za ujenzi wa tangi hilo ni Sh milioni 55 ukilinganisha na gharama za zaidi ya shilingi milioni 110 ambazo angezitumia mkandarasi, hivyo Muwasa iliamua kujenga yenyewe na kuokoa shilingi milioni 55 ambazo zitatumika kwa ajili ya shughuli nyingine za uendeshaji wa mamlaka baada ya ujenzi kukamilika Mei 30 mwaka huu. Kwa sasa kazi ya kusambaza maji tayari imeanza kwa kutandaza mabomba kwenda kwa wateja,” anafafanua Gantala.

Anaongeza: “Mpango huu hautoishia hapo tu, bali Muwasa tutaendelea kujenga matangi kwa nguvu zetu bila kutegemea zabuni za wakandarasi ili kupunguza gharama za ujenzi ambazo tungezitoa kwa wazabuni. Lengo letu ni kupanua mtandao wa maji na kuwafikia wateja wengi zaidi pale inapohitajika.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kusindika maji na maziwa cha Mara, James Mathayo anasema uzalishaji wa maji ya ziada kwa Muwasa kuanzia Septemba mwaka huu, ni habari njema kwa wawekezaji akiwemo yeye binafsi ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitumia maji ya visima vikubwa na virefu kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa kiwanda hicho.

“Uzalishaji wa maji ya Serengeti na kusindika maziwa ya Mara ambayo yamejizolea soko katika nchi za Tanzania na Kenya kutokana na ubora wake unahitaji maji ya kutosha. Hivyo itakuwa ni nafuu sana kwetu kibiashara tutakapopata maji safi, salama na yenye uhakika,” anasema. Mathayo.

 Anasema kutokana na uzalishaji unaofanywa na viwanda vingi vya bidhaa za hapa nchini na kuuzwa katika soko lenye ushindani la Jumuiya ya Afrika Mashariki kunaondoa dhana potofu iliyojengeka kwa baadhi ya wafanyabiashara toka nchi wanachama kuwa Tanzania haina cha kuuza katika soko hilo.

Kukamilika kwa mradi huo mkubwa maji wa Musoma kutaenda sambamba na fursa nyingine kwa wawekezaji katika miji ya Bunda na Serengeti ambako pia miradi miwili ya maji yenye thamani ya Sh bilioni 14 inayosimamiwa na Muwasa inatarajia kukamilika hivi karibuni, hivyo kuvutia pia wawekezaji katika miji hiyo.

Tayari wafugaji kutoka baadhi ya vijiji katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara wanaiomba Muwasa inayosimamia mradi wa maji wa Mugumu kuwawekea vituo maalumu vya maji vya kunyweshea mifugo yao ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima baina yao na wananchi wakiwemo wakulima wilayani humo.
 
Kiongozi wa wafugaji hao, Wilson Machota anasema kuwa kujengwa kwa vituo hivyo kutatoa fursa kwa wafugaji kuondokana na tatizo la upatikanaji wa vyanzo vya maji vya mifugo yao ambayo kwa muda mrefu sasa imekuwa ikilazimika wakati mwingine kutumia mabwawa na malambo ya maji yanayotumika kwa matumizi ya binadamu na shughuli za kilimo. Hali hiyo anasema imekuwa ikisababisha migogoro isiyo ya lazima baina yao na watumiaji wengine wa maji hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni