Rais mstaafu Jakaya
Kikwete akizindua mradi wa maji wa Mugumu katika hafla iliyofanyika kwenye
bwawa la maji la Manchira wilayani Serengeti Julai 2, mwaka 2010.
Imeandikwa na Bigambo Jeje
Imechapishwa: 01 Julai 2016
WAFUGAJI
kwenye baadhi ya vijiji katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara wameiomba
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) kuwawekea vituo vya
maji kunywesha mifugo ili kumaliza migogoro kati yao na wananchi wengine,
wakiwemo wakulima.
Kiongozi
wa wafugaji hao, Wilson Machota anatoa ombi hilo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
MUWASA, Said Gantala alipokagua ujenzi wa chujio la maji kwenye mradi wa maji
wa Mugumu (MUGUWASA) wilayani Serengeti. Ujenzi wa mradi huo ulianza Januari
15, 2015.
Machota anasema, kujengwa kwa vituo hivyo kutatoa fursa kwao kumaliza
tatizo la upatikanaji wa vyanzo vya maji kwa ajili ya mifugo. Kutokana na
tatizo hilo wakati mwingine wanatumia mabwawa ya maji ya binadamu na
kusababisha migogoro.
“Mapema
Machi 20 mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Jumanne
Maghembe alipotembelea bwawa la Machira lililojengwa na serikali kama chanzo
cha maji ya kuja hapa Mugumu alituonya sisi wafugaji kwamba tusiharibu vyanzo
vya maji na kwamba kwa kufanya hivyo tunahatarisha uhai wa vyanzo hivyo,”
anasema Machota.
Profesa Maghembe ameyasema hayo katika kijiji cha Rung’abure
wilayani baada ya kushuhudia wafugaji wakinywesha mifugo kwenye vyanzo vya
maji.
“Kwa
msingi huo ili tutekeleze kwa vitendo agizo hilo la serikali, hatuna budi
kujengewa mabirika maalumu ya maji kwa ajili ya mifugo yetu kama vile ng’ombe,
mbuzi, kondoo na punda ili kuondoa migogoro tunayokumbana nayo katika kutafuta
malisho na maji ya mifugo, na hii si kwetu tu Serengeti nadhani ni changamoto
kubwa pia kwa wafugaji katika mikoa mingine ya nchi yetu,”anasema.
“Jamani
mradi huu ni wa kwenu, lakini nilichokiona pale kwenye chanzo cha maji, ng’ombe
kwenye eneo chepechepe,” anasema Profesa Maghembe. “Jamani fanyeni juhudi au
lolote mnalofanya lakini msiingize ng’ombe kwenye chanzo cha maji na kama
mkiingiza basi maisha ya mradi yatakuwa mafupi na hakuna mtu wa kumlaumu kwa
sababu ni ninyi wenyewe mmekuwa kama mtu anayekata tawi la mti alilokalia,”
anasema.
Waziri
Maghembe anasema, katika eneo la mradi wa Rung’abure kuna mkulima analima
kwenye msitu jirani na chanzo cha maji cha mradi wa kijiji hicho.
Anasema,
mwananchi huyo anahatarisha chanzo hicho na amemtaka mkulima huyo baada ya
kuvuna asirudie tena kulima eneo hilo. Amemwagiza Mwenyekiti wa Kijiji ampe
mwananchi huyo shamba lingine. Amewataka wakulima wilayani Serengeti kuondoka
katika vyanzo vyote vya maji kwa vile wanavunja Sheria ya Mazingira Na 20 ya
mwaka 2004.
Kwa
mujibu wa sheria hiyo hairuhusiwi kulima mita 60 kutoka chanzo cha maji.
Amezitaka serikali za vijiji wilani Serengeti mkoani Mara pia kuhakikisha
zinasimamia suala la mifugo hususani ng’ombe ili wasipelekwe kunywa maji kwenye
eneo la chanzo cha maji.
Ametaka
mifugo hiyo ikanywe maji kwenye mabirika au malambo yaliyojengwa kwa ajili ya
mifugo. Mkazi wa mjini Mugumu tangu mwaka 1986, Christina Mauma anasema
kukamilika kwa mradi wa maji wa Mugumu kutoka bwawa la Manchira kutawezesha
mabadiliko ya kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kumaliza kero ya maji
iliyoiwakabili kwa zaidi ya miaka 30.
Mauma anasema, awali wakazi wa mji wa
Mugumu walitegemea maji kutoka kwenye visima vya asili vilivyopo maeneo ya
Magereza,Takuburya na Matunusi.
Kwa
mujibu wa mwananchi huyo, wakati wa kiangazi walilazimika kusubiri hadi usiku
wa manane ili kupata maji. “Wanawake wa mji wa Mugumu tuliteseka sana na
kutumia muda mwingi kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na hali
ilikuwa mbaya sana wakati wa majira ya kiangazi ndiyo hali ilitisha kabisa
maana ilitulazimu wakati mwingine kusubiria hadi wakati wa manane kupata maji
kutokana na visima hivyo kutoa maji kidogo sana,” anasema.
Mauma
anasema, mradi wa maji na usafi wa mazingira Mugumu utakapokamilika watapata
faida nyingi kwa kuwa licha ya kupata maji safi na salama pia wataweza
kuanzisha bustani za mboga na matunda.
Anazitaja faida nyingine kuwa ni kutunza
mazingira kwa kupanda miti, kuweka mazingira ya vyoo katika hali ya usafi na
kupata maji ndani ya mita 400 kama sera ya maji ya serikali ya mwaka 2002
inavyosema. Mradi huo unaogharimu shilingi bilioni mbili unatarajiwa kukamilika
Septemba 30 mwaka huu.
Mkurugenzi
Mtendaji wa MUWASA, Gantala anasema, wananchi wameanza kupata huduma ya maji
kupitia vituo maalumu wakati wanasubiria kuwekewa mtandao wa mabomba hadi
majumbani na kwenye taasisi. Gantala anasema, ujenzi wa bwawa la Manchira
umekamilika.
Mafanikio hayo yameibua shughuli za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na
ufugaji wa samaki, ufugaji wa nyuki na hifadhi ya misitu na wanyamapori.
Anasema,
kazi ya ufugaji wa samaki katika bwawa la Mugumu ilianza baada ya kukamilika
ujenzi wa bwawa mwaka 2009 kwa kupandikiza vifaranga 15,000 aina ya sato
(Tilapia) waliopatikana katika Kituo cha Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) Sota, wilaya
ya Rorya mkoani Mara.
Kazi ya kuwavua kwa majaribio imeanza, watarajiwa kuanza
kuuzwa kwa kati ya Sh 3,000 hadi 5,000 kwa kila samaki.
“Wakati
hatua za utekelezaji wa mradi zikiwa zimefikia hatua ya asilimia 62 hadi Machi
2016, kazi zinazofanyika au zilizofanyika katika mradi huo ni ujenzi wa seti ya
chujio la maji, kulaza mabomba ya maji sanjari na ujenzi wa tangi huku mradi
ukitarajia kutoa faida mbalimbali baada ya kukamilika kwake,” anasema Gantala.
Anataja
faida baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Mugumu kuwa ni pamoja na wakazi
wa mji wa Mugumu kupata maji safi na salama, kupungua kwa magonjwa ya
kuambukiza kikiwemo kipindupindu, MUGUWASA kuongeza mapato na kuongeza mtandao
wa upatikanaji wa maji kwa kufikia asilimia 90.
Gantala
anasema, uwekaji wa chujio ukikamilika utasaidia kuchuja maji na kuweka dawa
hivyo amewaomba wananchi kuhakikisha bwawa la Manchira linaendelea kutumika kwa
kipindi kirefu kwa kutunza mazingira ili maji yaliyopo yasipungue.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni