Imeandikwa na Bigambo Jeje.
Imechapishwa: 06 Juni 2016
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge akikata utepe kuzindua ujenzi wa tangi la
maji kata ya Rwamlimi mjini Musoma
MAMIA
ya maelfu ya wakazi wa Manispaa ya Musoma na wilaya ya Bunda mkoani Mara, siyo
muda mrefu wataanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama baada ya miradi
ya maji kukamilika.
Miradi
hiyo inatarajiwa kuzinduliwa kati ya Juni na Julai mwaka huu, hatua
utakayomaliza kwa kiwango kikubwa kero ya upatikanaji wa maji salama takribani
iliyodumu kwa muda mrefu.
Wakati
wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maji mkoani Mara mwezi Machi mwaka huu,
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, aliwaagiza wakandarasi wa miradi
hiyo ambao ni kampuni za Spencon na Mauza Nyakirang’ani, kuhakikisha
zinakamilisha kazi hizo ndani ya muda wa mkataba na tayari miradi hiyo
imekamilika kwa wastani wa zaidi ya asilimia 90.
Miradi
hiyo mikubwa ya maji iliyojengwa kwa ushirikiano baina ya wafadhili na
serikali, ni ahadi za serikali kwa wananchi zilizotolewa kwa nyakati tofauti na
serikali ya awamu ya nne iliyokuwa inaongozwa na Jakaya Kikwete kama sehemu ya
utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Miradi
hiyo ni pamoja na ule mradi mkubwa wa maji wa Musoma Mjini unaojengwa katika eneo
la Bukanga, kata ya Makoko unaotarajiwa kuanza kusukuma maji kwa wananchi
ifikapo Juni 30 mwaka huu na wa Nyabehu wilayani Bunda.
Wakati
mradi wa Bukanga umegharimu Sh bilioni 45 ule wa Nyabehu umegharimu Sh bilioni
10. Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa) ambaye
ofisi yake iliopewa jukumu la kusimamia miradi yote ya mamlaka za maji mkoani
Mara.
Said Gantala anasema miradi hiyo miwili sasa iko katika hatua za mwisho
kabisa na kwamba itakabidhiwa ndani ya miezi hii ya Juni na Julai mwaqka huu.
Gantala
anasema kukamilika kwa miradi hiyo kunahitimisha ule msemo wa Kiswahili usemao
kwamba “mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni” akimaanisha kwamba licha ya
kejeli za baadhi ya wanasiasa wa kambi ya upinzani, Rais mstaafu Kikwete daima
atakumbukwa na wananchi wa mkoa wa Mara kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwapatia
maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria sambamba na vyanzo vingine vya maji.
“Rais
mstaafu, Jakaya Kikwete alitoa ahadi hiyo wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa
mkoa wa Mara mjini Musoma Septemba 25 mwaka 2010 na kutoa ahadi kadha wa kadha
lakini suala la miradi ya maji alilipa kipaumbele zaidi na kuahidi kwamba
endapo angepewa ridhaa tena ya kuwaongoza Watanzania angelihakikisha miji ya
Musoma, Bunda, Mugumu, Tarime na miji midogo ya Mugango, Kiabakari na Butiama
inapata maji safi na salama,” anasema.
Gantala
anafafanua kwamba miradi yote hiyo ni ahadi za serikali kupitia utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 hadi 2015 kama ilivyoainishwa katika
ibara ya 86 (a), (e) na (i) zinazozungumzia kuongeza upatikanaji wa huduma ya
maji safi na salama kufikia asilimia 65 vijijini na mijini asilimia 75.
Anasema
kwamba mbali na serikali kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM, pia kupitia
Muwasa inatekeleza Sera ya Maji ya mwaka 2002 inayolenga katika kuhakikisha
kuwa, wananchi vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama umbali usiozidi
mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Anafafanua
kuwa madhumuni ya sera hiyo ni kuwezesha uendelezaji na usimamizi endelevu wa
utoaji wa huduma ya maji safi na uondoaji majitaka kwa wakazi wa mijini huku
madhumuni hayo yakifikiwa kwa kuweka malengo na kutoa miongozo na vigezo vya
utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na Mamlaka za Maji safi na Majitaka mijini
pamoja na watekelezaji wengine.
Aidha,
anasema sera hiyo ya maji inalenga katika masuala mbalimbali ikiwemo kutoa
mwongozo wa namna ya kuendeleza na kusimamia huduma ya majisafi na majitaka
mijini kwa ufanisi sambamba kuweka mazingira mazuri yatakayoivutia sekta
binafsi kuwekeza katika kutoa huduma ya majisafi na uondoaji majitaka mijini.
Mkurugenzi
huyo Mtendaji wa MUWASA anatabaisha kuwa madhumuni mengine katika sera hiyo ni
pamoja na kuhakikisha kuwa upo muundo mzuri wa kitaasisi unaovipa vyombo vya
uendeshaji huduma ya majisafi na majitaka mijini madaraka ya kujiendesha
vyenyewe kibiashara.
Hiyo
ni pamoja na kuwa na mfumo madhubuti na wenye ufanisi wa ukusanyaji maduhuli
yatokanayo na mauzo ya majisafi na uondoaji wa majitaka na hivyo kuongeza
mapato sanjari na kupunguza upotevu wa maji na kuboresha uondoaji wa majitaka.
Gantala
anafafanua kuwa kukamilika mwa miradi hiyo kutatoa nafuu kwa watumiaji wa maji
kwa kupunguza bei ya ankara za maji ili kutoa fursa kwa watu wengi kutumia
huduma hiyo muhimu.
Anaongeza
kwamba mradi mkubwa wa maji wa Musoma Mjini una tangi la maji litakalotumika
kusambaza maji katika kata za Rwamlimi na Bweri na kwamba tanki hilo linajengwa
kwa nguvu za Mamlaka ya Maji Musoma ambapo mamlaka hiyo inatarajia kuongeza
wateja 1,000 kupitia tangi hilo.
“Tangi
hilo lina ujazo wa lita 135,000 na litahudumia maeneo ya Rwamlimi, Songambele,
Songe na taasisi nne shule za sekondari na msingi na litatumika kama msaada wa
tanki kuu litakalojengwa eneo la Kwangwa.
Gharama
za ujenzi wa tanki hilo ni Sh milioni 55 lakini kama lingejengwa na mkandarasi
lingetumia zaidi ya Sh milioni 110, hivyo Muwasa imeokoa shilingi milioni 55
ambazo zitatumika kwa shughuli nyingine za uendeshaji wa mamlaka,” anasema.
Mkazi
wa kata ya Kamunyonge katika Manispaa ya Musoma, Tatu Kulwa anamshukuru Rais
mstaafu Kikwete kutekeleza ahadi yake ya kujenga mradi mkubwa wa maji katika
historia ya mji wa Musoma ambao licha ya kuwa kando ya Ziwa Viktoria umekuwa na
changamoto ya maji.
“Pamoja
na Muwasa kuboresha huduma zake za usambazaji wa maji katika mji wetu, mradi wa
Bukanga ndio unaenda kuwa mwarobaini wa kero ya maji yaliyokuwa yakisumbua hasa
kata za pembezoni mwa Manispaa ya Musoma kama vile Bweri, Rwamlimi, Nyakato,
Kigera, Kwangwa, Buhare na Nyamatare,” anasema.
Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Mara Christopher Sanya anatoa kwa hatua
iliyofikiwa na kusema anafarijika kuona ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya
2010 hadi 2015 inatekelezwa vyema.
Kuhusu
mradi wa Nyabehu, Sanya anasema utawanufaisha maelfu ya wananchi wa vijiji 14
ikiwa ni pamoja na wakazi wa halmashauri ya Mji wa Bunda. Vijiji hivyo 14
vyenye wakazi zaidi ya 150,000 vinavyonufaika na mradi huo ni pamoja na
Nyabehu, Mwiseni, Buzimbwe, Bulamba, Nyantare, Guta na Kinyambwiga. Vijiji
vingine ni Tairo, Migungani, Bunda Stoo, Balili, Nyamakokoto, Manyamanyama na
Sazira.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni