Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed
Gharib Bilal, akipata maelezo ya mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi wa
Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Musoma, Gantala Said, wakati wa sherehe za
Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa
Mkoani Mara jana Machi 22, 2015.
Imeandikwa na Bigambo Jeje.
Imechapishwa: 20 Januari 2016
MAMLAKA
ya Maji Safi na Taka ya Musoma Mjini (MUWASA) ni moja ya taasisi za umma ambazo
kama zitalipwa ipasavyo na wadeni wake, zinaweza kuboresha utendaji kazi wake
kuliko ilivyo sasa.
Wananchi
wengi wa mji wa Musoma ambao wamekuwa wakilalamikia huduma ya maji, wamekuwa
wakikutana na kauli ya ukata inayoisumbua mamlaka hiyo kutokana na kudai Sh
milioni 560 ambazo hazijalipwa na baadhi ya Taasisi za Serikali mkoani Mara
kutokana na taasisi hizo kulimbikiza ankra za huduma ya maji kwa muda mrefu.
Kutokana
na serikali ya Awamu ya Tano kuanza kazi kwa kuhimiza ukusanyaji mzuri wa
mapato na kubana matumizi, wengi sasa wana matumaini kwamba taasisi za serikali
ambazo zimekuwa zikilimbikiza madeni zitaanza kulipa madeni yao ili kuziwezesha
taasisi zingine zinazotoa huduma zimudu kutoa huduma nzuri zaidi.
Lima
Masinde, ambaye ni mteja wa kawaida wa Muwasa, anasema ili kutekeleza kwa
vitendo kaulimbiu ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu taasisi za serikali
zinazodaiwa na watu binafsi au taasisi zingine za serikali, hazina budi kulipa
madeni yao ili taasisi kama Muwasa ziweze kumudu kuwahudumia vyema wateja wao
wakiwemo wananchi wanaolipa kwa wakati.
Masinde
anasema kitendo cha baadhi ya taasisi za serikali kulimbikiza madeni ya huduma
ya maji kwa muda mrefu kinakwenda kinyume na sheria ya Maji Na 12 ya mwaka
2009, ibara ya 20 na 21 inayosisitiza umuhimu wa mteja kupewa maji na
kuhakikisha analipa kwa wakati bila shuruti, vinginevyo mteja anaweza
kufikishwa mahakamani. “Sheria ya Maji inayosimamiwa na serikali iko bayana
kabisa juu ya umuhimu wa kuhudumiwa na kuilipia huduma hiyo.
Hivyo
kwa kutumia sheria hiyo ni vyema mamlaka za juu, hata kama ni Rais Magufuli
aziagize wizara husika ambazo taasisi zake zinadaiwa kulipa madeni yao ili
kuikwamua mamlaka kujiendesha kwa ufanisi,” anasema.
Mteja
mwingine, Selemani Bakari, mkazi wa Nyasho, mjini Musoma anapokea taarifa hizo
kwa mshangao na kuhoji iweje wateja wa kawaida walipe ankara zao kwa wakati na
pale inapotokea kuchelewa kulipa baada ya mwezi mmoja tu Muwasa huwa inawakatia
huduma ya maji lakini kumbe kuna wateja wakubwa ambao wamelimbikiza madeni kwa
muda wa takriban mwaka mmoja sasa bila kulipa ankara zao. “Taarifa hizi kwa
ujumla zimenishitua sana.
Nashangaa
kusikia kwamba hata taasisi kama hospitali ya rufaa ya Musoma inayopokea ruzuku
kila mwezi kwamba nayo inadaiwa mamilioni ya pesa. Ninajua umuhimu wa maji kwa
hospitali na haipendezi kukata maji katika eneo nyeti kama hilo, lakini ni
vyema ikahakikisha inalipia huduma ya maji ili iendelee kupatikana,” anasema
Bakari.
Naye
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Mara, Maximillian Ngesi, anaamini kwamba kutokana
na kasi ya utendaji kazi wa Rais John Magufuli, serikali itaboresha kwa haraka
huduma zote za kijamii, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Muwasa inalipwa kwani ni
sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 hadi
2020.
Ngesi
anasema ili kutekeleza Sera ya Maji ya mwaka 2002 inayolenga katika kuhakikisha
kuwa, wananchi vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama umbali usiozidi
mita 400 kutoka kwenye makazi yao sambamba na huduma ya maji mijini, taasisi
hizo lazima zihakikishe zinalipa fedha zinazodaiwa kama njia ya kuiwezesha Muwasa
kuendelea kutoa huduma bora.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Muwasa, Said Gantala anathibitisha kuwepo kwa deni hilo na kuzitaja
taasisi zinazodaiwa kuwa ni pamoja na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa, Ofisi ya
Mkuu wa Magereza Musoma, Hospitali ya Rufaa ya serikali ya mkoa wa Mara pamoja
na Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Gantala anasema taasisi hizo zimeshindwa
kulipa madeni hayo na kuiweka pabaya mamlaka yake katika kuwahudumia wananchi
kwa vile Muwasa haipokei ruzuku yoyote ile ya kusaidia uendeshaji kama zilivyo
taasisi na idara nyingine za serikali zinazopata ruzuku kutoka hazina kila
mwezi.
Anasema
amejitahidi kwa kiasi kikubwa kukutana na wakuu wa taasisi hizo ili kuangalia
jinsi wangechukua hatua ya kuanza kulipa madeni yao kwa awamu lakini hadi sasa
hakuna hatua za utekelezaji zilizochukuliwa na wakuu hao.
“Sisi
kama mamlaka tayari tumeshatoa taarifa ya kusudio la mwezi mmoja la kuzifikisha
mahakamani taasisi hizo pale zitakaposhindwa kulipa madeni hayo na hatutasita
pia sasa kuzisitishia huduma ya maji bila kujali umuhimu wa watu wanaowahudumia
kama hospitali na magereza,” anasema.
Mkurugenzi
huyo Mtendaji wa MUWASA anafafanua kuwa hospitali ya rufaa ya serikali ya mkoa
wa Mara ndiyo inayoongoza kwa kudaiwa Sh milioni 176.5 ikifuatiwa na Ofisi ya
Kamanda wa polisi mkoa wa Mara inayodaiwa Sh milioni 175.9 huku Ofisi ya Mkuu
wa Magereza mkoa wa Mara na Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma wakidaiwa Sh
milioni 155.5 na Sh milioni 40.2.
Gantala
anakiri kwamba wakati wateja wao wa nyumbani na sehemu za kibishara wakilipa
kwa asilimia 100, tatizo liko kwa baadhi ya taasisi na ndio maana anaomba sasa
kila taasisi ya serikali inayodaiwa, si na Muwasa pekee bali na watoa huduma
zingine kulipa madeni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni