Jumanne, 2 Agosti 2016

MRADI WA MAJI WALETA FARAJA BUNDA




Imeandikwa na Bigambo Jeje
Imechapishwa: 18 Januari 2016 

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Bunda katika kijiji cha Nyabehu mkoani Mara Machi 20, 2015. Wa pili kushoto ni aliyekuwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na kushoto ni Mbunge wa Mwibara, Kange Lugora. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mara, Christopher Sanya, Mbunge wa zamani wa Bunda Stephen Wasira na Mkurugenzi wa kampuni ya Nyakirang’ani, Mauza Nyakirang’ani.  


KAMPUNI ya ujenzi ya Nyakirang’ani ya mjini Musoma mkoani Mara imeweza kutekeleza vyema mkataba wake na serikali wa ujenzi wa mradi wa maji wa Nyabehu wilayani Bunda ulioanza kutoa huduma kwa wananchi Oktoba 16, 2015.

Makala haya ya BIGAMBO JEJE inaelezea jinsi mradi huo ulivyoanza kunufaisha wakazi wa Bunda kiasi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara kuipongeza kampuni ya Nyakirang’ani kwa kufanikisha ujenzi huo kama mkataba ulivyotaka. 

WAKAZI zaidi ya 150,000 wa vijiiji 14 ukiwemo Mji wa Bunda mkoani Mara tangu Oktoba 16 mwaka jana, wamekuwa wakinufaika na huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya kukamilika kwa mradi huo wa maji wa Nyabehu uliotekelezwa kwa pamoja baina ya serikali na wahisani kupitia Benki ya Dunia (WB).

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya anatoa pongezi wakati akizungumzia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya 2010 hadi 2015 uliofanywa na serikali ukilenga kuwahudumia na kuwaletea maendeleo wananchi bila kujali itikadi zao kisiasa. 

Sanya anasema mradi huo wa Nyabehu uliogharimu Sh bilioni 10 na ulioko kata ya Butimba wilayani humo unaowanufaisha maelfu ya wananchi wa vijiji 14, ikiwa ni pamoja na wakazi wa halmashauri ya Mji wa Bunda umeleta faraja kwa wananchi waliokuwa wakisumbuliwa na tatizo la miaka mingi la upatikanaji maji kwenye maeneo yao.

Vijiji hivyo 14 vyenye wakazi zaidi ya 150,000 vinavyonufaika na mradi huo ni pamoja na Nyabehu, Mwiseni, Buzimbwe, Bulamba, Nyantare, Guta, Kinyambwiga, Tairo, Migungani, Bunda Stoo, Balili, Nyamakokoto, Manyamanyama na Sazira. 

Anasema amefurahishwa na kasi ya mkandarasi katika ujenzi huo, licha ya changamoto kadha wa kadha alizokumbana nazo wakati wote wa utekelezaji wa mradi na kuwataka wazabuni wengine hususani wazawa kuwa wavumilivu na wastahimilivu kama kampuni ya Nyakirang’ani walivyohimili changamoto zote walizokabiliana nazo na hatimaye kumaliza ujenzi huo.

“Mradi huo wa Nyabehu unaotoa maji yake Ziwa Victoria na ujenzi wake ulianza tangu 2006 kwa awamu na kuendelea tena rasmi mwezi Mei mwaka 2015 baada ya kusuasua kwa miaka mingi huko nyuma kutokana na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na wahisani na serikali kuchelewa kutoa fedha lakini baada ya fedha kupatikana utendaji kazi wa kampuni ya Nyakirang’ani umeenda kwa kasi na kuweza kukamilika,” anasema.

Mwenyekiti huyo wa CCM mkoani Mara anakiri kwamba kuchelewa kukamilika kwa mradi mapema kama ulivyokuwa umepangwa kulisababisha wananchi wengi kukata tamaa na kukiadhibu chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita wa Oktoba 25 mwaka jana kwa kukinyuma kiti cha ubunge wa jimbo la Bunda Mjini.

 “Ilifikia mahali ambapo watu wetu walikata tamaa na kupoteza matumaini kabisa juu ya mradi huu walioutegemea ukamilike miaka mingi iliyopita.

Baadhi walidhani tatizo lilikuwa ni kwa mkandarasi, lakini kumbe kukwama kwa mipango baina ya wahisani na serikali ndicho kilikuwa chanzo. Hii ilisababisha wananchi kutunyima kura katika uchaguzi wa mwaka jana,” Sanya anasema.

 Anaongeza: “Licha ya changamoto zote hizo za CCM kunyimwa kura katika uchaguzi mkuu wa 2015 katika jimbo la Bunda bado chama chetu kitaendelea kuwatumikia wananchi bila kujali itikadi zao za kisiasa kwa kuisimamia serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli na inayotokana na Chama Tawala cha Mapinduzi.”

Kwa niaba ya CCM, Sanya anawashukuru wahisani kwa jinsi wanavyoendelea kuiamini nchi kwa kutoa fedha zao kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo na kuelezea kwamba hiyo ni sifa njema kwa serikali jinsi gani inavyoaminika katika nyanja za kimataifa huku akiwataka wananchi kuitumia vizuri miradi yote iliyofadhiliwa na ama serikali au nchi wahisani.

 Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ujenzi ya Nyakirang’ani yenye makao yake makuu mjini Musoma mkoani Mara, Mauza Nyakirang’ani anakiri kukumbana na changamoto kadhaa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Anakumbusha kwamba jambo lolote la maendeleo na linalohusisha wadau wengi ni nadra kutokutana na changamoto. Mauza anasema lengo la ujenzi wa mradi huo ilikuwa ni kuondoa kero ya maji ya muda mrefu katika eneo hilo la wilaya ya Bunda na kwa kuwa kazi hiyo imemalizika kwa ufanisi na tija, sasa wananchi wameanza kupata maji safi na salama yeye hana budi ya kumshukuru kila mtu aliyeshiriki kwa namna moja ama nyingine katika kuhakikisha kwamba mradi huo unakamilika.

“Baada ya zoezi zima kwa sasa kuelekea kukamilika kwa asilimia 100, ni jambo la kuishukuru serikali na wahisani mbalimbali kupitia Benki ya Dunia kwa jnsi walivyojitoa kimasomaso na kuhakikisha kazi inaanza na kukamilika kama malengo ya mradi yalivyokuwa, suala la changamoto ni jambo la kawaida kwetu sisi wakandarasi hivyo daima hatukati tamaa,” anafafanua Mauza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Salama ya Musoma (MUWASA) inayosimamia miradi yote ya maji mkoani Mara, Said Gantala, anafafanua kwamba ujenzi wa mradi huo ni ahadi za Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 hadi 2015 kama ilivyoainisha katika ibara ya 86 (a) inayozungumzia kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kufikia asilimia 65 vijijini na mijini asilimia 75 ifikapo mwaka 2015.

Gantala anatanabaisha kuwa mbali na serikali kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM, pia kupitia Mamlaka za Maji zinatekeleza Sera ya Maji ya mwaka 2002 inayolenga katika kuhakikisha wananchi vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao. 

Anasema madhumuni ya Sera hiyo ni kuwezesha uendelezaji na usimamizi endelevu wa utoaji wa huduma ya majisafi na uondoaji majitaka kwa wakazi wa mijini. 

Kwa mujibu wa Gantala, sera hiyo ya Maji inalenga katika masuala mbalimbali, ikiwemo kutoa mwongozo wa namna ya kuendeleza na kusimamia huduma ya majisafi na majitaka mijini kwa ufanisi, sambamba kuweka mazingira mazuri yatakayoivutia sekta binafsi kuwekeza katika kutoa huduma ya majisafi na uondoaji majitaka mijini. 

Mkurugenzi Mtendaji huyo anasema baada ya kukamilika kwa mradi wa Nyabehu tayari serikali ilishamwagiza mhandisi wa Maji wilayani Bunda, Iddy Swai kuhakikisha anafanya mara moja upembuzi yakinifu wa njia za kujenga vituo vya kusambaza mabomba katika vijiji vya Buzimbwe, Mwiseni, Bulamba na Nyabehu vilivyopo kata ya Butimba katika jimbo la Mwibara, ambavyo serikali iliagiza viingizwe kwenye mradi kwa kuzingatia sera ya maji ya mwaka 2002 ya kuwapatia huduma wananchi wote wanaopitiwa na mradi wowote ule wa maji kwa vile wao ndo walengwa. 

Kwa upande wake, mkazi wa kijiji cha Buzimbwe, George Mambile anasema anaishukuru serikali kwa kusikia kilio chao na sasa wanaenda kupata huduma ya maji kwani hapo awali kijiji chao hakikujumuishwa kwenye vijiji nufaika. 

Naye Agnes Samsoni anasema serikali imewakumbuka na kwamba kupatikana kwa maji katika vijiji hivyo kutawaondolea adha ya maji inayowakabili kutokana na umbali mrefu wa kutoka kijijini hapo kwenda ziwani hususani wanawake ambao ndio waathirika wakubwa wa huduma hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni