KATIBU wa Mila wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya,
Mwanasimtwa Mwagongo amesema tukio la kupatwa kwa jua linalotarajiwa kutokea
leo katika Kijiji cha Rujewa wilayani hapa ni ishara ya Mwenyezi Mungu
kuukubali uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza Tanzania kutokea
tukio hilo tangu Aprili 18, 1977 na kwamba tukio kama hilo la kihistoria
linatarajiwa kutokea tena nchini Mei 21, 2031.
Mbali ya Rujewa ambako wataona kupatwa kwa jua
kwa asilimia 97 sawa na miji ya Makambako, Masasi, Mbeya, Tunduru, Njombe na
Sumbawanga, miji mingine ambayo itaona tukio hilo kwa ukaribu zaidi wa asilimia
96 ni Katavi, Nachingwea na Songea ikifuatiwa na Kigoma, Iringa, Mtwara na
Lindi.
Akizungumza jana na waandishi habari za Utalii na
Uwekezaji Tanzania (Tajati) nyumbani kwake katika Kata ya Isisi, Mwagongo
alisema tukio hilo la kupatwa kwa jua nchini si mkosi, bali ni sawa na taa
iliyokuwa imezimika na sasa imewashwa na kuongeza kuwa, ni ishara kuwa Mungu
ameukubali utawala uliopo madarakani na ndiyo sababu ametoa giza na kuleta
nuru.
Aliwaasa viongozi wa dini zote kote nchini
kuliombea tukio hilo ili lifanyike na kupita kwa amani na pasiwepo na uvunjifu
wa amani utakaosababisha jamii kutoa tafsiri ya tofauti baada ya tukio hili la
kihistoria ambalo litafanyika kati ya saa 4.15 asubuhi hadi saa 8.00 mchana.
Alisema baada ya tukio hilo, wazee wa kimila
watachinja ng’ombe kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa neema ya tukio hilo na pia
kumwomba aiepushe jamii na madhara yoyote yanayoweza kujitokeza.
“Hapo zamani watoto walikuwa hawaruhusiwi kutoka
nje siku ya tukio hili. Wazee waliamini ni ajali ya kugongana jua na mwezi na
wanaoumia ni wanadamu hasa watoto kwa kusababishiwa milipuko ya magonjwa
mbalimbali,” alisema katibu huyo na kuongeza:
“Lakini kwa sasa tunatambua kuwa ni tukio la
kisayansi na kutokea kwenye eneo letu ni neema kutoka kwa Mungu. Kupitia tukio
hili dunia itaijua Tanzania, itaijua Mbarali na itaijua Rujewa. Ni tukio ambalo
limetutangaza.”
Kwa upande wa walimu na wanafunzi katika shule
mbalimbali mjini Rujewa walionesha kuwa na furaha kubwa ya ujio wa tukio hilo
wakisema watapata fursa nzuri ya kujifunza kwa vitendo kwa kuwa watajionea
badala ya kusimuliwa au kusoma kwenye vitabu.
Mwalimu wa taaluma katika Shule ya Msingi Isisi,
Donatha Nkwera alisema walimu shuleni hapo wamewaandaa wanafunzi kwa ajili ya
tukio hilo linalotokea jirani na shule yao.
HABARI HII NI KWA HISANI YA GAZETI LA HABARI LEO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni