Pichani : Mkurugenzi wa MUWASA Said Gantala akitoa maelezo mafupi ya mradi wa maji kwa Mkuu wa wilaya ya Musoma Dk Vicent Naano na viongozi wa kidini na vyama vya siasa.
Imechapishwa: 05 Septemba 2016
Gazeti: Habari Leo
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA)
iliyopo mkoani Mara inatarajia kuanza ujenzi wa mtandao wa maji kwa lengo la
kupeleka huduma hiyo katika vijiji 21 vya Wilaya za Musoma vijijini na Butiama
vya kata 4 zinazozunguka Manispaa ya Musoma hivyo kuwaondolea kero ya
upatikanaji wa maji wananchi wa vijiji hivyo.
Taarifa hiyo inatolewa kwa Mkuu wa
Wilaya ya Musoma mkoa wa Mara Dk Vicent Naano na Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA
Said Gantala wakati wa ziara ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini na Vyama vya
Siasa walipotembelea na kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa
Musoma unaojengwa eneo la Bukanga kata ya Makoko.
Gantala anawaeleza viongozi hao kuwa Mradi
huo wa Majisafi Musoma unatekelezwa chini ya ufadhili wa Serikali ya Tanzania
kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AfD) na kwamba unagharimu
jumla ya shilingi bilioni 45 na unatekelezwa na kampuni ya ukandarasi ya Degremont-Spencon Consortium.
Anasema mkataba wa mradi huo ulisainiwa Novemba
06 mwaka 2012 na mkandarasi alianza kazi mwezi Desemba mwaka huo huo wa 2012 na
hadi sasa utekelezaji wa ujenzi wa mradi ukiwa umefikia asilimia 80 huku mradi
ukiwa umechelewa kwa mwaka mmoja kutokana na mkandarasi kukosa uwezo wa
kuendelea na ujenzi.
“ Hata hivyo Mkandarasi amerudi kazini
baada ya kupata mkopo kutoka Benki ya Standard Charter pamoja na msaada kutoka
kwa mshirika wake kampuni ya Degremont. Hivyo mradi unatarajiwa kukamilika
Mwezi November 2016, na kukabidhiwa
Mwezi December 2016” Anasema Gantala.
Anasema mpango huo ni katika kutekeleza
Sera ya Maji ya mwaka 2002 inayolenga katika kuhakikisha kuwa, wananchi
vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama umbali usiozidi mita 400 kutoka
kwenye makazi yao sambamba huduma ya maji mijini inayosimamiwa na kutekelezwa
na Mamlaka za Majisafi na Usafi Mazingira katika miji mikuu ya mikoa,Mamlaka
katika ngazi za Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa ya Maji.
Anafafanua kuwa madhumuni ya Sera hiyo
ni kuwezesha uendelezaji na usimamizi
endelevu wa utoaji wahuduma ya majisafi na uondoaji majitaka kwa wakazi wa
mijini huku madhumuni hayo yakifikiwa kwa kuweka malengo na kutoa miongozo na
vigezo vya utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na Mamlaka za Majisafi na
Majitaka Mijini na watekelezaji wengine, kwa nia ya kuboresha huduma ya utoaji
majisafi na uondoaji majitaka mijini.
Mkurugenzi huyo Mtendaji wa MUWASA
anavitaja vijiji hivyo 21 vitakavyonufaika na mradi huo mkubwa wa maji kwamba
ni pamoja na Etaro, Busambara, Nyegina, Mkirira, Kurukerege, Nyakatende, KigeraItuma,
Kakisheri, Kamuguruki, Kabegi, Nyasaungu, Kiemba, Nyabange, Nyankanga,Mmazami,Bukabwa,Bisumwa,Nyarukoru,Kyamajoje
na Nyabekwabi toka halmshauri za wilaya za Musoma Vijijini na Butiama mkoani
Mara.
“Maelfu ya wananchi wa vijiji hivi sasa
wataondokana na kero ya upatikanaji wa maji safi na salama iliuokuwa
ikiwakabili kwa mihongo kadhaa iliyopita hasa nyakati za majira ya kiangazi
ambapo mar azote vyanzo vingi vya maji ama upungukiwa maji kwa kiasi kikubwa au
kukauka kabisa hivyo kuleta adha kubwa ya upatikanaji wa maji” anasema na
kuongeza kwamba,
“Hatua hiyo sasa itasaidia kuvutia
wawekezaji mbalimbali wakiwemo wale wa viwanda vikubwa na vidogo vya usindikaji
wa samaki, mbogamboga na matunda sanjari na bidhaa za aina tofauti za vyakula
kuwekeza katika maeneo hayo ya vijijini yaliyo na rasilimali mbalimbali na
kusaidia kukuza pato na uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla”.
Gantala anazitaja faida za mradi huo
watakazozipata wananchi wa Manispaa ya Musoma pindi utakapokamilika kuwa ni
pamoja na upatikanaji wa Maji safi na salama kwa saa 24 kwa siku kwa asilimia
98, ongezeko la mtandao wa mabomba ya maji katika maeneo ambayo yalikuwa
hayapati maji sambamba na maeneo yaliyokuwa yanapata kwa mgao sasa watapata
muda wote huku huduma hiyo ikitarajia kupunguza magonjwa ya mlipuko
yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi na salama.
Faida nyingine ni MUWASA kuongeza
ufanisi kwa kuongeza uzalishaji maji toka mita za ujazo 10,000, za sasa na
kufikia mita za ujazo 34,000 kila siku, Kuongeza mapato ya Mamlaka kutoka
milioni 200 kwa mwezi hadi milioni 400 kwa mwezi ifikapo 2018/19, Huduma za
maji kuwa Bora zaidi na kufikia viwango vya kimataifa sanjari na kubooresha
maslahi ya Watumishi hivyo kuongeza mzunguko wa kiuchumi katika Manispaa ya
Musoma.
Anatanabaisha kwamba ujenzi wa mradi huo
umekabiliwa na changamoto kadha wa kadha muda wote wa ujenzi na kusababisha
hadi mradi kuchelewa kukamilika huku changamoto hizo zikiwa ni zile za mafundi
kukutana na mwamba mkubwa chini ya ardhi hivyo kuchelewesha kazi na kuchelewa
na hata kukataliwa kwa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kunakochelewesha upatikanaji wa vifaa vya
ujenzi mapema.
“ Kutokuwa na watumishi wa kutosha
kufanya kazi katika Mradi, Migogoro ya upatikanaji wa Kokoto za Mradi, Mgogoro
wa Menejimenti ya Mkandarasi kuchelewsha kazi, Kubadilishwa kwa njia ya mabomba
makubwa na Upatikanaji wa viwanja vya ujenzi wa mradi hasa matenki ya maji ni
changamoto nyingine ambazo zimejitokeza wakati wa ujenzi huu wa mradi mkubwa”
Anafafanua.
Baadhi ya viongozi wa madhebu ya dini
wanapongeza hatua iliyofikiwa na serikali katika ujenzi wa mradi huo mkubwa
utakaoanza kuwahudumia wakazi wapatao 150,000 wa Manispaa ya Musoma kwa mujibu
wa sense ya watu na makazi ya mwaka 2012 na kusema sasa wanayo matumaini
makubwa ya kuondokana na tatizo hilo la maji katika makazi yao.
Mmoja wa viongozi hao ni Mchungaji wa
Kanisa Kuu la Wasabato Jimbo la Mara la Kamunyonge Gerald Nyakirere anasema kwa
muda wa miaka mingi huduma ya maji katika Manispaa ya Musoma imekuwa ni
changamoto ya muda mrefu hususani katika kata za pembezoni za
Buhare,Kigera,Kwanga,Kamunyonge na Nyamatare lakini kwa hali ya ujenzi wa mradi
ulipofikia inaleta matumaini makubwa kwa wananchi.
“ Baada ya kukabiliwa na tatizo hili la
upatikanaji wa maji katika Manispaa yetu, sasa tunalo tumaini kubwa sana kwamba
watu wetu hasa kwa akina mama watakuwa na ahueni na kuondokana na usumbufu
walioupata kwa muda mrefu wa kadhia hii ya maji punde mradi huu tulioutembelea
utakapokamilika mwezi Desemba mwaka huu” anasema Mchungaji Nyakirere.
Akizungumzia
mipango ya ujenzi wa mradi mpya wa Maji Taka katika Manispaa ya Musoma
utakaogharimu zaidi ya sh bilioni 40 na unaotegemewa kuanza mwezi Novemba 2016,
Mkurugenzi wa MUWASA Gantala anasema unalenga kutengeneza mfumo wa Majitaka kwa
eneo la katikati ya Manispaa ya Musoma na unafadhiliwa na serikali kwa kushirikiana na wahisani wawili, AfD na
EIB pamoja kwa mkopo nafuu.
Anasema mradi
huo utajenga mabwawa ya kutupa majitaka, utalaza mabomba ya kusafirisha
majitaka toka katika majumba ya watu kupeleka katika mabwawa ya majitaka, mradi
utajenga vituo 4 vya kusukuma majitaka sambamba na kujenga vyoo 58 katika shule
za msingi na sekondari za Manispaa ya Musoma na kila choo kitakuwa na matundu
9.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni