Ijumaa, 23 Septemba 2016

MUSOMA YAELEKEA KUJINASUA NA TATIZO LA MAJITAKA



 
Imeandikwa na Bigambo Jeje
Imechapishwa: 22 Septemba 2016 
Gazeti: Habari Leo.


BAADA ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara kutokuwa na magari ya kunyonya majitaka kwa zaidi ya miaka 15, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa) inaelekea kutoa ufumbuzi wa tatizo hilo.

Mamlaka hiyo imekamilisha mipango ya ujenzi wa mradi mpya wa Majitaka katika Manispaa hiyo utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni 40, huku ujenzi wake ukitegemewa kuanza Novemba mwaka huu.

Mkurugenzi wa Muwasa, Said Gantala, anasema mradi huo unalenga kutengeneza mfumo wa majitaka kwa eneo la katikati ya Manispaa ya mji huo unaofadhiliwa na serikali kwa kushirikiana na wahisani wawili, Shirika la Maendeleo la nchini Ufaransa (AfD) na Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (EIB) kwa mkopo nafuu.

Gantala anasema mradi huo utahusisha ujenzi wa mabwawa ya majitaka na kulaza mabomba ya kusafirishia majitaka hayo toka katika majumba ya watu kupeleka katika mabwawa. Halikadhalika anasema mradi utajenga vituo vinne vya kusukuma majitaka sambamba na vyoo 58 katika shule za msingi na sekondari zilizopo katika Manispaa ya Musoma ambapo kila choo kitakuwa na matundu tisa.

“Huu ni mradi mkubwa wa majitaka ambao utaleta nafuu kubwa kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma ambao kila kukicha wanalazimika kukodi magari ya watu binafsi kwa ajili ya kunyonya maji machafu yakiwemo ya vyooni," anasema na kuongeza kwamba, 

“Kwa bahati mbaya wanaomudu kulipia huduma hizo ni watu wachache wenye uwezo wa kifedha. Anasema mradi huo utakapokamilika hakutakuwa na sababu ya kukodi magari tena kwani majitaka yataondolewa majumnbani na kwenye taasisi mbalimbali kwa mabomba hadi kwenye mabwawa”.

Anasema kwa vile idadi kubwa ya wananchi katika manispaa hiyo hawana uwezo wa kupata fedha za kulipia huduma hiyo, matokeo yake wanaamua kukiuka sheria za usafi wa mazingira na kutiririsha hovyo maji machafu mitaani, hususan kwenye mitaro.

Anasema hali hiyo inasababisha uchafuzi wa mazingira na kuleta hofu ya kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu.

Mkurugenzi huyo wa Muwasa anasema kukamilika kwa mradi huo wa majitaka itakuwa ni faraja kubwa sana kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma wapatao 150,000 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kwa kupata mfumo wa kisasa wa kusafirisha majitaka kutoka kwenye makazi na taasisi za umma na binafsi. 

Gantala anaamini kwamba hatua hiyo itaifanya Manispaa kuwa na miundombinu bora na ya kudumu, mintarafu suala zima la majitaka na hivyo kuwa chachu ya kutunza na kuhifadhi mazingira katika hali ya usafi.

Jumanne Magafu, mkazi wa kata ya Nyasho anakiri kwamba mji wa Musoma ambao huko nyuma ulikuwa ukiongoza kwa usafi nchini, sasa umekuwa ukikabiliwa na tatizo la uchafu linalochangiwa na watu kuriririsha hovyo maji machafu mitaani. 

Anasema mradi huo umekuja katika wakati mwafaka kwani anazijua baadhi ya taasisi zikiwemo za shule za msingi na sekondari katika mji huo zinazokabiliwa na matatizo makubwa ya upungufu wa vyoo, upatikanaji wa maji safi na pia namna ya kushughulikia majitaka yanayozalishwa.

Ofisa Afya Mkuu mstaafu wa Manispaa ya Musoma, Peter Mtaki, anasema hatua hiyo inaweza kusaidia kurejesha historia ya usafi wa mazingira ya miaka ya tisini ambapo Musoma ilishika nafasi ya kwanza hapa nchini kwa miaka mitatu mfululizo. 

Anafafanua kuwa miaka ambayo Halmashauri ya mji wa Musoma iliongoza mfululizo kwa usafi kitaifa ni 1992, 1993 na 1994.

Mtaki anasema mradi huo utakuwa wa kihistoria na utaleta mafanikio makubwa katika usafi wa mazingira kwa kuwa kwa miaka mingi walitegemea magari ya kunyonya maji machafu kutoka katika Halmashauri ya Mji (kabla ya kuwa manispaa) ambayo baadaye yaliharibika na kufanya watu binafsi kuhodhi huduma hiyo. 

Wananchi ambao vyoo vyao hujaa wamekuwa wakilazimika kupata huduma ya kunyonyewa majitaka kwa gharama ya kati ya Sh 80,000 na 100,000.

“Halmashauri wakati huo ilikuwa chini ya uongozi wa aliyekuwa Meya wa Mji, Eliasafu Lima. Ilipata mafanikio hayo kutokana na mikakati kadha wa kadha iliyojiwekea na kuitekeleza kwa vitendo pamoja na ushirikiano mkubwa baina ya watumishi wa afya na wananchi," anasema.

Ofisa afya huyo mstaafu anasema mara ya mwisho mji wa Musoma kushika uongozi wa usafi kitaifa ni mwaka 2002. “Mradi huu wa Majitaka unaoanza kujengwa mwezi Novemba mwaka huu utasaidia kuirejesha Manispaa kwenye historia ya kuwa vinara wa usafi katika nchi yetu kama sisi tulivyofanya miaka hiyo,” anasema Mtaki.


MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni