Na Bigambo Jeje,Musoma
Askofu wa Kanisa la Waadventista
Wasabato (SDA) jimbo la Mara Baba Daud Makoye amewataka wanasiasa na
wanaharakati wote kutoliingiza taifa katika vurugu na machafuko wakati huu
wa mchakato wa kutafuta katiba mpya na
badala yake wahakikishe katiba hiyo inapatikana kwa njia ya amani na wala si
vinginevyo.
Askofu Makoye ametoa wito huo mjini
Musoma siku ya Jumamosi katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa mwaka wa Makambi ulioandaliwa na makanisa sita ya
Wasabato ya Mtaa wa Mwisenge katika jimbo hilo laMara.
Amesema suala la kutafuta katiba mpya ni
jambo jema na lenye maslahi kwa Watanzania wote wenye itikadi mbalimbali za
kisiassa,kidini,kikabila,kiuchumi na kijamii hivyo mchakato wake unahitaji
kutanguliza maslahi ya watu wote na si ya watu wachache tu huku utunzaji wa
amani ya nchi ukitakiwa kupewa kipaumbele zaidi kuliko kitu chochote kile.
Amesema kwamba wanasiasa na wanaharakati
wa haki za binadamu katika baadhi ya nchi hapa duniani walitumia fursa za
michakato kama hiyo kuvuruga amani na kusababisha machafuko katika nchi zao kwa
tamaa za fedha,mali na madaraka jambo ambalo amekemea vikali kuwa halitakiwi
kabisa kutokea kwa nchi yenye kisiwa cha amani kama Tanzania.
Amefafanua kuwa vurugu
na machafuko yaliyojitokeza kwa majirani zetu wa Kenya mwaka 2007 sanjari na kutoweka kwa amani katika
nchi za Somalia,DRC Kongo na Nigeria ni fundisho kwa Tanzania kwamba hatuna
budi kuchezea amani iliyopo sasa na kutakiwa kuilinda kwa gharama ya aina
yoyote maana hakuna mbadala wake.
Kwa msingi huo Askofu
huyo wa kanisa la Waadventista Wasabato jimbo la Mara ametanabaisha kuwa kanisa
hilo linaungana na watanzania wote kuomba kwa Mungu amani ya nchi hii iendelee
kudumu kwa ajili ya ustawi wa watu wote huku akiongeza kwamba hakuna maendeleo
yoyote yale yatakayopatikana bila kuwepo kwa amani.
Baba Askofu Makoye amesema kupatikana kwa katiba mpya kwa njia ya amani
kutaendelea kuijengea heshima kubwa nchi yetu katika mataifa mbalimbali
duniani ambapo Tanzania inajivunia kumaliza mambo yake ya ndani kimya kimya
bila kuhitaji misaada ya ama mataifa makubwa au jumuiya za kimataifa tofauti na
nchi nyingine ambazo zinahitaji kusaidiwa kutatua migogoro yao ya ndani.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni