Na Bigambo Jeje-Tarime.
Watu wanne, wakiwamo raia watatu wa
Kenya wameuawa kwa tuhuma za ujambazi katika kijiji cha Mriba tarafa ya Ingwe
wilaya ya Tarime mkoa wa Mara unaopakana na nchi hiyo jirani ya Kenya.
Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa aliwataja waliouawa kuwa ni raia hao wa Kenya kutoka vijiji vya Ntimaro na Girabose wilaya ya Kurya East, Mwita Rugena (30), Rogona Nyamahoyi na Machera Marwa na Sagire Gachanga (25) wa kijiji cha Itiryo tarafa ya Ingwe wilayani Tarime Mkoa wa Mara.
Kamishina Msaidizi wa Polisi Mambosasa alisema kuwa mauaji hayo yalitokea Agosti 8 mwaka huu baada ya watuhumiwa hao waliokuwa na silaha kukutwa na wananchi wakitaka kupora fedha na simu za wateja katika duka la Shadrack Mahenye kijiji hapo Agosti 3, mwaka huu na kuwajeruhi kwa risasi watu watatu.
Alisema baada ya taarifa hizo, polisi wakwenda katika eneo la tukio na kuwakuta watuhumiwa hao wameuawa kwa kushambuliwa kwa kipigo n a wananchi.
"Miili ya watu hao imehifadhiwa hospitali ya wilaya ya Tarime ikisubiri kuchukuliwa na ndugu zao. Kwa sasa tunawahoji watu nane kuhusiana na mauaji hayo,” alisema Kamanda huyo na kuwataja kuwa ni wakazi wa Kijiji cha Mriba.
Wakati huo huo Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamsaka Mkazi wa kijiji cha Kanji tarafa ya Kirua Vunjo wilaya ya Moshi Vijijini , aliyejulikana kwa jina moja la Maurice kwa tuhuma za kumuua mwanawe mwenye umri wa miaka minne, Nicholaus Maurice (4).
“Siku mbili kabla tulimisikia baba yake akitamka kwa jazba wakati akimuadhibu mwanawe kwa kuchelewa kupeleka kijiko ili ale chakula na mke wake," alidai mmoja wa watu kwenye familia hiyo na kuongeza kuwa:
" Nitakuuwa ili niishi na mke wangu vema na usinipotezee malengo bora ufe, sikuhitaji tena," Alisema kuna uwezekana wa baba huyo kuwa wakati akimuadhibu mtoto huyo alimnyonga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo Agosti 10, mwaka huu saa 5 asubuhi.
Boaz alisema mtoto huyo alikutwa amefariki dunia baada ya kupigwa na baba yake mzazi huku mkono wake wa kushoto na makalio vikiwa vimevimba.
Alisema baada ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa huyo alitokomea kusikojulikana na kwamba polisi wanamsaka kwa udi na uvumba ili akamatwe na kufikishwa mahakamani.
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa hospitali ya Kilema ukisubiri kufanyiwa uchunguzi kisha kukabiliwa kwa ndugu kwa maziko.
“Inauma sana kuona mzazi unamchapa mtoto wako tena wa kumzaa paka umauti unamkuta, huu ni unyama. Tutahakikisha tunamsaka mzazi huyo popote pale alipo ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake” alisisitiza Kamanda Boaz.
Vilevile alisema Agosti 9, mwaka huu majira ya saa 6:15 usiku, Nastori Christian (60), alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitali ya Huruma iliyopo Rombo- mkuu, wilayani Rombo baada kudaiwa kupigwa kichwani kwa fimbo na mtoto wake, Christofa Nestori(25).
Kamanda Boaz alisema chanzo cha mtoto huyo kuamua kumchapa baba yake huyo hakijajulikana, hivyo wanamshikilia kwa mahoajiano zaidi. Imeandikwa na Jumbe Ismailly, Singida, Samson Chacha, Tarime na Mary Mosha, Moshi.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni