Na Bigambo Jeje,Musoma
Chama cha Mapinduzi(CCM) katika wilaya
ya Musoma kimemtaka mbunge wa jimbo la Musoma Mjini Mhe:Vicent Nyerere kuacha
kujipatia umaarufu kisiasa kwa kuendelea kulaghai na kupotosha wananchi juu ya
ukweli wa miradi ya maendeleo iliyoahidiwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano
Mhe:Dk Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM Taifa
(NEC) Mhe:Vedastus Mathayo ametoa kauli hiyo wakati akihutubia maelfu ya
wananchi wa Manispaa ya Musoma katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama
hicho na kufanyika katika uwanja wa shule ya msingi Mukendo.
Mathayo amesema kuwa mbunge huyo amekuwa
akiendelea kutumia vibaya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika jimbo la
Musoma Mjini iliyoahidiwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe:Kikwete kwa wakazi wa
Musoma Mjini alipokuwa akinadi ilani ya CCM katika uchaguzi mkuu uliopita.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa
barabara kwa kiwango cha lami kati ya Musoma na Lamadi mkoa wa Simiyu yenye
thamani ya sh.bilioni 85 ujenzi ambao uko katika hatua za mwisho, ujenzi wa
mradi mkubwa wa maji safi na salama toka Ziwa Victoria wenye thamani y
ash.bilioni 14 sanjari na uendelezaji wa ujenzi wa hospitali ya kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Kwangwa ambayo kwa pamoja iliahidiwa Dk Kikwete
na imetekelezwa na serikali yake.
Mjumbe huyo wa NEC amemtaka Mhe:Myerere
kuacha upotoshaji huo na badala yake awaeleze wapiga kura wake ametekelezaje
ahadi zake lukuki alizoahidi katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo baadhi ya
ahadi hizo zilikuwa ni pamoja na kusambaza mtandao wa maji katika mitaa yote ya
Musoma Mjini baada ya kuuza magari ya serikali ya sekta ya maji aliyodai hayana
faida kwa wananchi.
Mathayo amezitaja ahadi nyingine
zinazotakiwa kutekelezwa na mbunge huyo ni zile za kutoa ajira kwa vijana
katika vyombo vya dola kama vile uhamiaji,polisi,magereza na JWTZ, kufuta
ushuru kwa wafanyabishara wadogo,kutengeneza madawati katika shule zote za
msingi na sekondari, kubomoa na kujenga upya barabara za lami katika Manispaa
ya Musoma ahadi ambazo hajawahi kuanza kuzitekeleza hata kwa sehemu ndogo tu.
Kwa msingi huo amewataka wananchi wa
Musoma Mjini kuachana na propaganda za kiongozi huyo juu ya miradi ya maendeleo
inayoendelea kutekelezwa na serikali kwamba inatokana na ilani ya uchaguzi ya
CCM chini ya Rais Dk Jakaya Kikwete licha ya chama hicho kutopewa ridhaa ya
Ubunge na madiwani katika uchaguzi wa 2010 ambapo chama cha CHADEMA kilipewa
ridhaa hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni