Na Bigambo Jeje,Musoma.
Kanisa la Waadventista la Wasabato(SDA)
jimbo la Mara limewataka Watanzania kuombea amani iliyopo hapa nchini ili
iendelee kudumu, hivyo kulisaidia taifa kuepukana na matukio ya ugaidi na vita vya
wenyewe kwa wenyewe vinavyozikumba baadhi ya nchi za Afrika na kwingineko
duniani.
Mwinjilisti Mlei wa kanisa hilo Asheri
Mukama ametoa kauli hiyo mjini Musoma August 02 mwaka huu katika kanisa la
Wasabato la Kamunyonge wakati akiendesha
ibada maalum ya changizo la fedha za mkutano wa injili wa makambi unaotarajiwa kufanyika katika kanisani hapo kati ya mwezi August 17 hadi August 23 mwaka huu.
Mukama amesema kwamba Watanzania wote
bila kujali itikadi zao kidini,kisiasa na kikabila hawana budi kuendelea
kuombea amani ya taifa hili iliyoasisiwa na marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere na kuifanya nchi kuheshimika katika medani ya kimataifa kwa kuwa kisiwa
cha amani.
Amesema kuwa matukio ya kigaidi ya
Alshabab yanayozitesa nchi za Kenya,Uganda na Somalia sanjari na kundi la
kigaidi la Boko Haramu nchini Nigeria huku makundi ya waasi yakizisumbua nchi
za Rwanda na DRC Kongo ni fundisho kwa Tanzania kwamba hatuna budi kuchezea
amani iliyopo sasa na kutakiwa kuilinda kwa gharama ya aina yoyote maana hakuna
mahali inapopatikana tena ikiuzwa mara tu inapotoweka.
Amesema dunia kwa hivi sasa inashuhudia
damu nyingi za watu wasio na hatia zikimwagika bure katika matukio ya ugaidi
sambamba na vita na kutishia amani kutoweka katika nchi nyingi,hali ambayo
amesema inasababishwa na kuongezeka kwa uasi na kupungua kwa upendo miongoni
mwa wanadamu mambo yanayotakiwa kuepukwa na wananchi wote wenye mapenzi mema na
nchi hii.
Akizungumzia suala la Katiba mpya,
Mwinjilisti Mlei Mukama ameisihi kamati ya maridhiano ya bunge maalum la Katiba
aliyoiunda Mwenyekiti wa bunge hilo Mhe:Samweli Sitta kuweka mbele mustakabali na maslahi ya nchi kwanza kuliko
kitu kingine chochote kile na kukubaliana kupitisha katiba itakayoendelea
kuweka misingi mizuri ya amani huku akiwataka wabunge wa UKAWA kurejea bungeni kuendelea
na mjadala wa rasimu ya katiba mpya.
Aidha Mwinjilisti huyo Mlei amesema
kupatikana kwa katiba mpya kwa njia ya amani kutaendelea kuijengea heshima
kubwa nchi yetu katika mataifa
mbalimbali duniani ambapo Tanzania inajivunia kumaliza mambo yake ya ndani
kimya kimya bila kuhitaji misaada ya ama mataifa makubwa au jumuiya za kimataifa
tofauti na nchi nyingine bali ni kinara wa kusaidia kutatua migogoro ya
majirani zake pale inapoombwa kufanya hivyo.
MWISHO.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni