Pichani ni Mchungaji wa Kanisa la Wasabato Mtaa wa Kamunyonge Muso Stehen Muso akiwa katika moja ya mahubiri yake katika kanisa hilo (Picha na Bigambo Jeje)
Na Bigambo
Jeje,Musoma
Kanisa la Waadventista
la Wasabato (SDA) la Kamunyonge la Mjini Musoma ambalo ni kanisa Kuu katika jimbo
la Mara, limeunga mkono hatua ya serikali ya kufuta utaratibu wa vyuo vikuu
mbalimbali hapa nchini kuwalazimisha wanafunzi kufanya mitihani katika siku zao
za ibada hususani siku ya jumamosi.
Mchungaji wa kanisa
hilo kuu la SDA la Kamunyonge Stephen Muso amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, hatua hiyo itawaondolea kero
ya kuabudu wanafunzi waliokuwa wakilazimishwa kuhudhuria makongamano na kufanya
mitihani katika siku zao za ibada hivyo kuingilia uhuru wao wa kuabudu na
kuvunja katiba ya nchi.
Mchungaji Muso amesema
kwa mujibu wa ibara ya 19 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977 inatoa uhuru wa mtu yeyote kuabudu bila shuruti na akatanabaisha kwamba
mazoea yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya walimu katika vyuo hivyo ilikuwa ni
ukiukwaji na uvunjaji wa moja kwa moja wa
sheria ya nchi.
Amesema kanisa la
Waadventista Wasabato limeamua kutoa pongezi hizo kwa serikali inayoongozwa na
Rais Dk Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kupokea malalamiko toka kwa baadhi ya
wanafunzi na kwa kuzingatia ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG)
ukafanyiwa kazi na kutolewa uamuzi bila kusita.
Serikali imesema
imeamua kwa dhati kabisa kuchukua hatua hiyo baada ya kuwepo kwa malalamiko
mengi ya wanafunzi toka vyuo mbalimbali wakihoji kwanini walazimishwe kufanya
mitihani siku za mwisho wa juma badala ya siku za kawaida za kazi hatua
iliyowafanya baadhi yao kusitisha masomo na kurudi nyumbani kwa uhuru wao dini
kuingiliwa pasipo sababu zozote za msingi.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika waraka wake wa Novemba 11 2014 kwenda kwa
Makamu na Wakuu wote wa vyuo vikuu na Vishiriki amewataka kuachana kabisa na
utaratibu huo wa mazoea ya kuwafanyisha mitihani wanafunzi siku za ibada zao
kwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu na uvunjaji wa katiba ya nchi.
Kwa mujibu wa waraka
huo wenye Kumb Na: ED/OKE/NE/VOL.1/01/49 uliyosainiwa kwa niaba yake na C.P
Mgimba utatoa uhuru wa kuabudu hata kwa wale wanafunzi waliokubali kufanya hivyo
kwa shingo upande tu huku wakihofia ama kufukuzwa vyuo kwa kutoifanya mitihani
hiyo au kuogopa kuidai haki yao ya kimsingi kama ilivyobainishwa katika katiba
ya nchi.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni