Jumapili, 9 Novemba 2014

RAIS KIKWETE AFANYIWA UPASUAJI WA TEZI MAREKANI

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania akibadilishana mawazo na mmoja wa madaktari bingwa wa hospitali ya Johns Hopkins muda mfupi kabla ya kufanyiwa oparesheni yake (Picha na IPP Media).



Rais Jakaya Kikwete, amefanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostrate) katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salvatory Rweyemamu, Rais Kikwete alifanyiwa upasuaji huo juzi alfajiri.

Taarifa ya Rweyemamu ilieleza kuwa upasuaji huo ulichukua takribani saa moja na nusu na kwamba ulifanyika salama na kwa mafanikio makubwa.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais Kikwete alifanyiwa upasuaji huo baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake kujiridhisha kuwa alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo.

“Hali ya Mheshimiwa Rais Kikwete inaendelea vizuri, bado yuko wodini akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa wananchi wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais Kikwete kwa kadiri zitakavyokuwa zinapatikana.

Rais Kikwete aliondoka Alhamisi ya wiki iliyopita kwenda nchini Marekani huku taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ikieleza kuwa Rais alikuwa anakwenda Marekani kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba Rais Kikwete atakuwa nchini humo kwa siku 10.

CHANZO: GAZETI LA NIPASHE


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni