Jumatatu, 3 Novemba 2014

MFUKO WA BIMA YA AFYA WALETA MADAKTARI BINGWA MARA







Pichani: Meneja huduma za Afya wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Dr Michael Kishiwa akitoa maelezo mafupi wakati wa uzinduzi wa huduma za madaktari bingwa mkoani Mara inazofanyika kwa siku sita mfululizo kwenye hospitali ya serikali ya mkoa ( Picha Na Bigambo Jeje).




Na Bigambo Jeje,Musoma


Serikali mkoani Mara imesema kuwa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Mwalimu Nyerere unaoendelea kwa fedha za serikali ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete utapunguza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za afya toka kwa madaktari bingwa kwa wananchi wa Mara na mikoa ya jirani.


Mganga mkuu wa mkoa wa Mara Dk Samson Winani amesema ujenzi huo unaoendelea katika eneo la Kwangwa katika Manispaa ya Musoma uko katika hatua nzuri na kuongeza kwamba utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya watoto na wanawake wanaofariki dunia ama kwa kukoswa madaktari bingwa walioko katika hospitali za rufaa au fedha kwa ajili ya kutafuta huduma hiyo.

Dk Winani ametoa kauli hiyo wakati akiwakaribisha jopo la madaktari 10 toka hospitali za rufaa za Muhimbili jijini Dar es Salam,Bugando jijini Mwanza sanjari na wale wa kutoka hospitali ya serikali ya mkoa wa Mara akiwemo yey mwenye ambao wametumwa na wizara ya afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutoa huduma kwa siku sita kwa wagonjwa mbalimbali wanaosumbuliwa na magonjwa yaliyoshindikana kutibiwa katika hospitali za kawaida.

Amesema serikali mkoani Mara inatoa pongezi za dhati kwa Rais Kikwete kutimiza ahadi yake kwa wananchi wa mkoani hapa kama alivyoahidi Septemba 25 mwaka 2010 alipohutubia maelfu ya wananchi na kuwaambia juu ya nia yake ya kuukwamua ujenzi huo uliokuwa umekwama tangu mwishoni mwa miaka ya themanini baada ya fedha za kuendeleza jengo hilo kukosekana.

Rais Jakaya Kikwete kutekeleza ahadi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama chake cha Mapinduzi(CCM) ya mwaka 2010-2015 ibara ya 85 (f) inayosema serikali itaendeleza jitihada za kujenga uwezo wa ndani wa kutoa huduma ya matibabu ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu hususani kwa maradhi ya moyo, figo, mishipa ya fahamu na saratani.

Kwa upande wake Meneja wa huduma za Afya wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Dk Michael Kishiwa amesema mfuko huo utatumia vifaa tiba na dawa vyenye thamani y ash milioni 4 katika zoezi hilo litalohudumia wananchi wa magonjwa yenye kuhitaji madaktari bingwa toka wilaya sita za mkoa wa Mara ambazo ni pamoja na Musoma,Butiama,Serengeti,Bunda,Tarime na Ryoya.

Dk Kishiwa amesema lengo la huduma hiyo itakayotolewa pia katika mikoa mingine ya hapa nchini ni kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi na kutatua kero za maradhi yanayowasumbua baada ya kukoswa tiba mbadala kutokana na kukoswa fedha za kuwapata madaktari bingwa ambao wengi wao wako katika hospitali za rufaa pekee.

MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni