Jumanne, 6 Desemba 2016

MAJI YA SERENGETI YAVUTIA WATALII HIFADHI YA TAIFA


Na Bigambo Jeje, Musoma.

Kiwanda cha kusindika maziwa na maji cha Mara Dairy kilichopo mjini Musoma mkoani Mara  kimeanza kujipanga kukabiliana na ushindani wa soko la maji ya kunywa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuendelea kuzalisha bidhaa bora sanjari na kutumia bidhaa za kiwanda hicho kutangaza  vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.


Moja ya mkakati ulioanzishwa na kiwanda hicho katika kukabiliana na ushindani wa soko la bidhaa hiyo katika nchi za EAC ni kubadili jina la maji toka Super Water na kuwa Serengeti ambayo ni moja ya hifadhi kubwa ya wanyama katika bara la Afrika na iko kwenye maajabu saba duniani.

Jumatatu, 7 Novemba 2016

SAMUEL SITTA HATUNAE TENA











Pichani Mhe:  Rais John Magufuli alipomtembelea ili kumjulia hali Marehemu Samuel Sitta hivi karibuni kabla ya kifo chake, nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam




Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, Samuel Sitta (74) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo jijini Munich nchini Ujerumani.

Mtoto wa marehemu, Benjamin Sitta amekaririwa akisema kuwa, mwanasiasa huyo ameaga dunia saa 10:00 usiku wa kuamkia leo.

‘’Nikweli mzee amefariki nchini Ujerumani akiwa anapatiwa matibabu, alipelekwa Alhamisi iliyopita na alikuwa anasumbulia na saratani ya tezi dume ambayo ilisambaa na kuathiri miguu na mwili mzima." amesema Benjamin.

Rais John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai.
“Nitamkumbuka Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za siasa na Serikali.

“Kupitia kwako Mhe. Spika naomba kutoa pole nyingi kwa Mke wa Marehemu Mhe. Magreth Sitta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Urambo na familia nzima ya marehemu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi wa Urambo Mkoani Tabora na watu wote walioguswa na msiba huu” amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.

Sitta alizaliwa Desemba 18, 1942 wilayani Urambo mkoa wa Tabora.



( Habari hii ni kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la Habari Leo)

Ijumaa, 23 Septemba 2016

VIJIJI 21 MUSOMA NA BUTIAMA KUNUFAIKA NA MAJI SAFI


Pichani : Mkurugenzi wa MUWASA Said Gantala akitoa maelezo mafupi ya mradi wa maji kwa Mkuu wa wilaya ya Musoma Dk Vicent Naano na viongozi wa kidini na vyama vya siasa.



Imechapishwa: 05 Septemba 2016
Gazeti: Habari Leo

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) iliyopo mkoani Mara inatarajia kuanza ujenzi wa mtandao wa maji kwa lengo la kupeleka huduma hiyo katika vijiji 21 vya Wilaya za Musoma vijijini na Butiama vya kata 4 zinazozunguka Manispaa ya Musoma hivyo kuwaondolea kero ya upatikanaji wa maji wananchi wa vijiji hivyo.

Taarifa hiyo inatolewa kwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma mkoa wa Mara Dk Vicent Naano na Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA Said Gantala wakati wa ziara ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini na Vyama vya Siasa walipotembelea na kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa Musoma unaojengwa eneo la Bukanga kata ya Makoko.

MUSOMA YAELEKEA KUJINASUA NA TATIZO LA MAJITAKA



 
Imeandikwa na Bigambo Jeje
Imechapishwa: 22 Septemba 2016 
Gazeti: Habari Leo.


BAADA ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara kutokuwa na magari ya kunyonya majitaka kwa zaidi ya miaka 15, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa) inaelekea kutoa ufumbuzi wa tatizo hilo.

Mamlaka hiyo imekamilisha mipango ya ujenzi wa mradi mpya wa Majitaka katika Manispaa hiyo utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni 40, huku ujenzi wake ukitegemewa kuanza Novemba mwaka huu.

Mkurugenzi wa Muwasa, Said Gantala, anasema mradi huo unalenga kutengeneza mfumo wa majitaka kwa eneo la katikati ya Manispaa ya mji huo unaofadhiliwa na serikali kwa kushirikiana na wahisani wawili, Shirika la Maendeleo la nchini Ufaransa (AfD) na Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (EIB) kwa mkopo nafuu.

Gantala anasema mradi huo utahusisha ujenzi wa mabwawa ya majitaka na kulaza mabomba ya kusafirishia majitaka hayo toka katika majumba ya watu kupeleka katika mabwawa. Halikadhalika anasema mradi utajenga vituo vinne vya kusukuma majitaka sambamba na vyoo 58 katika shule za msingi na sekondari zilizopo katika Manispaa ya Musoma ambapo kila choo kitakuwa na matundu tisa.

“Huu ni mradi mkubwa wa majitaka ambao utaleta nafuu kubwa kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma ambao kila kukicha wanalazimika kukodi magari ya watu binafsi kwa ajili ya kunyonya maji machafu yakiwemo ya vyooni," anasema na kuongeza kwamba, 

“Kwa bahati mbaya wanaomudu kulipia huduma hizo ni watu wachache wenye uwezo wa kifedha. Anasema mradi huo utakapokamilika hakutakuwa na sababu ya kukodi magari tena kwani majitaka yataondolewa majumnbani na kwenye taasisi mbalimbali kwa mabomba hadi kwenye mabwawa”.

Anasema kwa vile idadi kubwa ya wananchi katika manispaa hiyo hawana uwezo wa kupata fedha za kulipia huduma hiyo, matokeo yake wanaamua kukiuka sheria za usafi wa mazingira na kutiririsha hovyo maji machafu mitaani, hususan kwenye mitaro.

Anasema hali hiyo inasababisha uchafuzi wa mazingira na kuleta hofu ya kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu.

Mkurugenzi huyo wa Muwasa anasema kukamilika kwa mradi huo wa majitaka itakuwa ni faraja kubwa sana kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma wapatao 150,000 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kwa kupata mfumo wa kisasa wa kusafirisha majitaka kutoka kwenye makazi na taasisi za umma na binafsi. 

Gantala anaamini kwamba hatua hiyo itaifanya Manispaa kuwa na miundombinu bora na ya kudumu, mintarafu suala zima la majitaka na hivyo kuwa chachu ya kutunza na kuhifadhi mazingira katika hali ya usafi.

Jumanne Magafu, mkazi wa kata ya Nyasho anakiri kwamba mji wa Musoma ambao huko nyuma ulikuwa ukiongoza kwa usafi nchini, sasa umekuwa ukikabiliwa na tatizo la uchafu linalochangiwa na watu kuriririsha hovyo maji machafu mitaani. 

Anasema mradi huo umekuja katika wakati mwafaka kwani anazijua baadhi ya taasisi zikiwemo za shule za msingi na sekondari katika mji huo zinazokabiliwa na matatizo makubwa ya upungufu wa vyoo, upatikanaji wa maji safi na pia namna ya kushughulikia majitaka yanayozalishwa.

Ofisa Afya Mkuu mstaafu wa Manispaa ya Musoma, Peter Mtaki, anasema hatua hiyo inaweza kusaidia kurejesha historia ya usafi wa mazingira ya miaka ya tisini ambapo Musoma ilishika nafasi ya kwanza hapa nchini kwa miaka mitatu mfululizo. 

Anafafanua kuwa miaka ambayo Halmashauri ya mji wa Musoma iliongoza mfululizo kwa usafi kitaifa ni 1992, 1993 na 1994.

Mtaki anasema mradi huo utakuwa wa kihistoria na utaleta mafanikio makubwa katika usafi wa mazingira kwa kuwa kwa miaka mingi walitegemea magari ya kunyonya maji machafu kutoka katika Halmashauri ya Mji (kabla ya kuwa manispaa) ambayo baadaye yaliharibika na kufanya watu binafsi kuhodhi huduma hiyo. 

Wananchi ambao vyoo vyao hujaa wamekuwa wakilazimika kupata huduma ya kunyonyewa majitaka kwa gharama ya kati ya Sh 80,000 na 100,000.

“Halmashauri wakati huo ilikuwa chini ya uongozi wa aliyekuwa Meya wa Mji, Eliasafu Lima. Ilipata mafanikio hayo kutokana na mikakati kadha wa kadha iliyojiwekea na kuitekeleza kwa vitendo pamoja na ushirikiano mkubwa baina ya watumishi wa afya na wananchi," anasema.

Ofisa afya huyo mstaafu anasema mara ya mwisho mji wa Musoma kushika uongozi wa usafi kitaifa ni mwaka 2002. “Mradi huu wa Majitaka unaoanza kujengwa mwezi Novemba mwaka huu utasaidia kuirejesha Manispaa kwenye historia ya kuwa vinara wa usafi katika nchi yetu kama sisi tulivyofanya miaka hiyo,” anasema Mtaki.


MWISHO.

Alhamisi, 1 Septemba 2016

MWENYEZI MUNGU KAMKUBALI MAGUFULI






KATIBU wa Mila wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Mwanasimtwa Mwagongo amesema tukio la kupatwa kwa jua linalotarajiwa kutokea leo katika Kijiji cha Rujewa wilayani hapa ni ishara ya Mwenyezi Mungu kuukubali uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.

Jumapili, 21 Agosti 2016

MUSOMA EXPRESS NA CATA MINING ZATOA MISAADA YA SH BILIONI 1.2 MUSOMA

Na Bigambo Jeje,Musoma.
Agosti 3 2016.
MISAADA.

Pichani ni moja ya Mabasi mapya 18 ya kampuni ya Mabasi ya Musoma Express yanayotoa huduma za usafiri katika mikoa mbalimbali ya hapa nchini. 

Makampuni ya mabasi ya Musoma Express na Mgodi wa madini wa CATA uliopo wilaya ya Butiama mkoani Mara yametoa misaada ya zaidi ya sh bilioni 1.2 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kusaidia shughuli za maendeleo ya kijamii katika sekta mbalimbali kwa lengo la kupunguza umasikini na kukuza uchumi wa wananchi.