Jumatatu, 8 Septemba 2014

MAJONZI,SIMANZI VYATAWALA VIUNGA VYA MANISPAA MUSOMA



Baadhi ya maelfu ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wakiingia na kutoka chumba cha kuhifadhia maiti kutambua miili ya ndugu,jamaa na marafiki katika hospitali ya serikali ya mkoa wa Mara (Picha Na Bigambo Jeje)


Na Bigambo Jeje,Musoma

Watu wapatao 36 wamefariki dunia mkoani Mara baada ya mabasi mawili ya abiria kugongana uso kwa uso eneo la Sabasaba siku ya Ijumaa  Septemba 5 mwaka huu nje kidogo ya Manispaa ya Musoma huku ajali hiyo ikisababisha majeruhi79
 
Baadhi ya majeruhi katika ajali hiyo ni waandishi wa habari wawili wa mkoani Mara Frolence Focus wa gazeti la Mwananchi na Pendo Mwakyembe wa kituo cha redio cha Victoria Fm cha mjini Musoma ambao wote wamelazwa katika hospitali ya serikali ya mkoa wa Mara iliyopo mjini hapa.
 
Wakizungumzia tukio hilo mashuhuda wa ajali hiyo iliyohusisha basi la Mwanza coach lililokuwa likitokea Musoma kwenda Mwanza na basi la J4 likitokea Mwanza kwenda Sirari ambayo namba  hazikuweza kufahamika mara moja kugongana uso kwa uso majira ya saa 5 asabuhi.
 
Walisema mabasi hayo ambayo yote yalikuwa kwenye mwendo kasi yalikutana kwenye daraja dogo katika eneo hilo huku pia gari dogo aina ya Land Cruiser  likitaka kuovateki na hivyo kupelekea kutokea kwa ajali hiyo.
 
Mmoja wa mashuhuda hao aliyejitambulisha kwa jina la Juma Nyamhanga alisema alisikia kishindo kikubwa muda mfupi baada ya kutokea kwa ajali hiyo na baadae kusikia vilio vikitokea ndani ya mabasi hayo.
 
“Kwa kweli ni ajali mbaya sana ambayo sijapata kuiona kwenye maisha yangu,magari haya yamekutana eneo la daraja na pia kulikuwa na gari dogo eneo hilo nadhani kila moja lilitaka kupita eneo hilo na kujikuta yamegongana na kuongeza kuwa,
 
“Hili basi la Mwanza coach lilikuwa likitokea Musoma na J4 lilikuwa likitokea Mwanza na yalikuwa kwenye mwendo kasi nadhani hiyo ilikuwa ni sababu kubwa ya kutokea kwa ajali hiyo”.
 
Mganga mkuu wa mkoa wa Mara Dk Samsoni Winani amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyohusisha mabasi mawili ya abiria ya Mwanza Coach na J4 Express na kupokelewa kwa miili ya watu waliokufa na wale waliojeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea saa 5 asubuhi wakati mabasi hayo yakitokea kati ya miji ya Mwanza na Musoma.
 
Dk Winani amewataja baadhi ya waliofariki katika ajali hiyo kwamba ni pamoja na Dk Anatoria Ntangeki wa hospitali ya serikali ya mkoa wa Mara na mfanyakazi wa idara ya kilimo na mifugo mkoani Mara Juma Sayi Mambina waliofia hapo hapo kwenye ajali.
 
Hata hivyo amesema bado miili ya watu wengine 27 waliofariki dunia katika ajali hiyo haijatambuliwa na ndugu,jamaa na marafiki wao sanjari na majeruhi wengine 46 kwa kile alichosema taarifa rasmi itatolewa na ofisi yake hapo baadaye baada ya kutoa huduma za tiba kwa majeruhi.
 
Maelfu ya kwa maelfu ya wakazi wa katika Manispaa ya Musoma wamemwagika katika hospitali ya serikali ya mkoa wa Mara ilipo miili ya watu waliokufa na majeruhi wa ajali kwenda kushuhudia watu waliohusishwa ajalini huku vilio,majonzi na simanzi vikizizima kila kona na kila upande na baaadhi yao wakizimia baada ya kupata taarifa za familia zao.
 
Mama mmoja mwenye umri wa kati ya miaka 40 na 50 ambaye jina lake halikufahamika mapema alisikika akilia kuwa amepoteza watoto wake wawili waliokuwa wakisafiri kuelekea jijini Mwanza kwenye sherehe ya harusi waliokuwa abiria wa basi la Mwanza Coach lililokuwa likitoka Musoma kwenda jijini humo.
 
Ajali nyingine kubwa kutokea katika eneo hilo na kupoteza maisha ya watu ilitokea mwaka 1995 ambapo ilihusisha basi la Busigasore lenye nambari za usajili TZD 3444 aina ya Isuzu liligonga gari dogo na kupinduka mji mdogo wa Kiabakari na kuua watu 35 hapo hapo huku watu zaidi ya 45 wakijeruhiwa wengi wao vibaya.
 
                                              MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni