Pichani ni sehemu ya shamba la mahindi la mmoja wa wakulima walionufaika na mkopo wa mbolea ya Minjingu ttarafa ya Nyanja Musoma Vijijini (Picha na Bigambo Jeje)
Na Bigambo Jeje,Musoma
Taasisi ya mfuko wa uwekezaji kiuchumi
katika tarafa ya Nyanja(NEIT) iliyopo halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini
mkoani Mara mwezi Septemba mwaka huu
itatoa mikopo ya pikipiki 245 yenye thamani ya sh.milioni 563.5 ikiwa ni
mkakati wake wa kupambana na upunguzaji wa tatizo la ajira na umasikini kwa
wananchi.
Kutolewa kwa mkopo huo utakuwa ni
mwendelezo wa mfuko wa NEIT kuendelea kuwekeza miradi mbalimbali yenye thamani
ya sh bilioni 52 ndani ya kipindi cha miaka 10 baada ya mwezi June mwaka huu
kutoa mkopo wa mifuko 600 ya mbolea aina ya minjingu yenye thamani ya sh.milioni
19 kwa wakulima wa halmashauri hiyo kupitia vikundi vyao vya ujasriamali.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya NEIT bw.
Steven Machumu amesema hadi kufikia Desemba mwaka huu taasisi hiyo itakuwa
imetoa mkopo wa pikipiki zipatazo 1000 kupitia vikundi 32 vilivyoomba kupewa
mkopo huo wenye thamani ya sh bilioni 2.3 ingawa hadi hivi sasa idadi ya
waliojaza fomu za maombi ni watu 446.
Bw.Machumu amesema walengwa wa mkopo huo
watatoa sh.laki tatu kwa kila mwombaji na mkopo huo utakuwa wa kati ya miezi 13
na 18 kwa riba ndogo ya asilimia 9 ambapo marejesho ya mkopo yatakuwa ni sh
elfu thelathini kwa wiki au laki moja na ishirini kwa mwezi.
Amesema wananchi walioanza kunufaika na
miradi hiyo ya NEIT ya kupambana na hali ya umasikini ni wananchi wa kata za
Bukumi, Nyambono, Suguti, Nyegina, Bukima, Murangi,Kiriba,Makojo,Busambara,Bulinga,Kiriba,Tegeruka
na Butata huku akiwataka baadhi ya wanasiasa wanaozunguka katika tarafa hiyo na
kuwalaghai wananchi kwamba wasirejeshe mikopo hiyo kwa madai kuwa inatolewa
bure waachane kabisa na propaganda za aina hiyo.
Amesema taasisi hiyo aina chembe yoyote
ile ya itikadi ya kisiasa,kidini wala kikabila lakini ameshangazwa na hatua ya
baadhi ya wanasiasa wenye uchu wa madaraka kutaka kukwamisha shughuli za
maendeleo ya wananchi kwa kuihusisha na itikadi za kisiasa bali waeleze mipango
yao yenye manufaa kwa wakazi wa Nyanja bila kuingilia kazi za mfuko huo.
Bw. Machumu amesema NEIT itasaidia
kupunguza umasikini wa wananchi wa kata 17 za halmashauri ya wilaya ya Musoma
Vijijini katika sekta za Kilimo,Uvuvi,Ufugaji,Mazingira,Elimu na Afya ambapo
miradi mikubwa kupitia sekta hizo imeanza kutekelezwa katika kipindi cha miaka
mitano ya mradi ulioanza mwaka huu wa fedha wa 2013/14.
Amesema lengo la uwekezaji huo ni kuleta
mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi walio wengi vijijini wanaoabiliwa na umaskini
mkubwa ambapo baadhi ya miradi mikubwa iliyolengwa kutekelezwa katika mkakati
huo ni mapinduzi ya kijani katika sekta ya kilimo kwa kushirikiana na serikali
katika mpango wake wa KILIMO KWANZA kupitia ASDP na DADIPS.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni