Jumanne, 23 Septemba 2014

MHAGAMA AWATAKA WATANZANIA KUTOWACHAGUA WAPINZANI WA NYERERE

Pichani:Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi bibi Jenisita Mhagama akiwasha mshumaa kwenye kaburi la Baba wa Taifa Mwitongo Butiama. (Na Bigambo Jeje)




Na Bigambo Jeje,Butiama

Naibu wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bibi Jenister Mhagama amewataka Watanzania kutowachagua viongozi wanaochochea vurugu na fujo kwa wananchi, zenye nia ya kutowesha amani ya nchi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere wakati tunapoelekea katika uchaguzi wa mkuu hapo mwakani.

Naibu Waziri Mhagama ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kuzulu kaburi la Marehemu Mwalimu Nyerere kijijini kwake Mwitongo Butiama wilayani Butiama mkoani Mara ambapo alifuatana na viongozi wa juu wa Chuo Kikuu Huria(OUT) wakiongozwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Tolly Mbwete.


Amesema Mwalimu Nyerere daima atakumbukwa na wapigania amani katika bara zima la Afrika na duniani kote kwa kutumia muda na rasilimali zake kutafuta amani huku akiiwekea nchi yetu misingi ya kudumu ya kuilinda amani hivyo akawataka wananchi kamwe wasiwachague katika uchaguzi mkuu ujao, viongozi na wanaharakati wanaotaka kuivuruga amani kwa tamaa zao za madaraka kwa kuwa ni wapinzani wa moja kwa moja wa Baba wa Taifa.

Amesema kwamba kutokana na  mchango wa marehemu Mwalimu Nyerere katika medani ya amani duniani,jumuiya za kimataifa zikiongozwa na uliokuwa Umoja wa nchi huru za Afrika(OAU) zilimpa jukumu la kuzisaidia nchi zilizokuwa chini ya utawala wa kikoloni kuzikomboa nchi hizo kupitia tume ya ukommbozi iliyoongozwa na Marehemu Brigedia Jenerali Hashimu Mbita.

Naibu Waziri huyo ambaye pia ni mbune wa jimbo la Peramiho (CCM) amewataka Watanzania watakaopiga kura katika uchaguzi mkuu ujao mbali na kutowachagua viongozi wenye kukinzana na maadili ya Mwalimu Nyerere wawapuuze,wawakatae na kuwazomea kwa vile wanataka kuleta machafuko na kuifanya nchi isitawalike na watu washindwe kufanya kazi zao za maendeleo.

Kauli hiyo ya Jenister Mhagama imetolewa siku chache baada ya Chama cha  Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chini ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe kikitangaza kufanya maandamana nchi nzima na migomo isiyo na kikomo iko ili kulishinikiza bunge la katiba kuvunjwa kwa kile wanachodai bunge hilo ni batili.

Wakati CHADEMA wakitoa msimamo huo, Jeshi la Polisi nchini, nalo limesisitiza kuwa maandamano hayo ni batili na yamelenga kuchochea vurugu hivyo mwanachama au mtu yeyote ambaye atashiriki, atakamatwa na kuchukuliwa hatua.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi alipata fursa ya kuzindua kituo cha Chuo Kikuu Huria cha mkoa wa Mara kilichokarabatiwa kwa sh.milioni 220 huku akiwataka wanawake kujitokeza kupata elimu ya juu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia badala ya kuendelea kulalamikia kutopewa fursa mbalimbali ukiwemo uongozi ndani ya taasisi na serikalini.

MWISHO.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni